KUTUNGWA KWA SHERIA YA UFILISI KUTAPUNGUZA CHANGAMOTO ZA MFUMO WA UFILISI NCHINI
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akiongea mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Dkt. Joseph Mhagama akiongea wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya RITA kuhusu mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa uratibu wa majukumu ya usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu, Ufilisi na Udhamini
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas
Ndumbaro amesema Taasisi nyingi zimekuwa zinafanya ufilisi nchini kutokana na
kuwa na sheria nyingi za ufilisi, hivyo kukiwa na sheria ya ufilisi moja
kutawezesha Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) waendelee na shughuli
yake ya ufilisi kwani ndiyo Taasisi pekee iliyopewa jukumu la ufilisi.
Hayo ameyasema wakati Afisa Mtendaji Mkuu
wa RITA Bi. Angela Anatory akiwasilisha taarifa kuhusu mafanikio na changamoto
katika utekelezaji wa uratibu wa
majukumu ya usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu, Ufilisi na Udhamini kwa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria leo Oktoba 27, 2022 jijini
Dodoma.
Katika taarifa hiyo RITA wamependekeza
kutungwa kwa sheria ya Ufilisi ili kuweza
kukabiliana na changamoto zinazoukabili mfumo wa ufilisi nchini.
Akitaja changamoto hizo katika taarifa yake
Bi. Anatory amesema uwepo wa sheria nyingi zinazosimamia ufilisi nchini ni moja
ya changamoto inayowakabili katika mfumo wa ufilisi.
Ameongeza kuwa Uwepo wa mamalaka nyingi za
usimamizi wa masuala ya ufilisi, sheria kutoainisha taratibu za ufilisi
unaovuka mipaka, kutokuwepo kwa chombo cha kusimamia wataalam wa ufilisi na
kukosekana kwa usalama wa malipo ya waajiriwa wakati wa ufilisi wa kampuni ni
miongoni mwa changamoto zinzoikabili Wakala katika utekelezaji wa jukumu lake
la Ufilisi.
Bi Anatory amesisitiza kuwa Serikali
iangalie namna gani taasisi zake zitabadilishana taarifa na kutunziana mifumo
kwa gharama nafuu kwani huduma hiyo kwa sasa imekuwa ikitolewa kwa gharama
kubwa.
Afisa Mtendaji huyo pia ameelzea huduma zao
za usajili wa vizazi, vifo, ndoa, talaka na watoto wa kuasili na udhamini namna
ambavyo zimefanikiwa kutokana na elimu inayotolewa kwa jamii na kampeni mbazo
wamekuwa wakizifanya katika Mikoa mbalimbali.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Katiba na Sheria Dkt. Joseph Mhagama ameishukuru wizara namna ambavyo
inaishirikisha kamati katika mambo mbalimbali na hivyo kuiwezesha Kamati hiyo
kupata uelewa wa kutosha kuhusu majukumu yake.
Miongoni mwa mambo yaliyohitaji ufafanuzi
kutoka kwa Wabunge ni pamoja na umri
sahihi wa kuoa na kuolewa, suala la mirathi, usajili wa vizazi na changamoto ya
sheria ya ufilisi. Dkt. Ndumbaro alitoa ufafanuzi na kuahidi maelezo zaidi
yatatolewa kwa maandishi.
Comments
Post a Comment