MAWAKILI WA SERIKALI TEKELEZENI MAJUKUMU YA SERIKALI KWA KUZINGATIA SHERIA – DKT. NDUMBARO
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza na Mawakili wa Serikali wakati akifunga mkutano wa siku tatu wa Mawakili hao jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo (kushoto) na Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA Bi. Angela Anatory wakifuatlia hotuba ya kufunga Mkutano wa Mawakili wa Serikali.
Mawakili wa Serikali wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi.
XXXXXXXXXXXXXXXX
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas ndumbaro amewaasa
Mawakili wa Serikali kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria kwa
maendeleo ya nchi.
Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo wakati akifunga mkutano Mkuu wa
Mawakili wa Serikali leo tarehe 30 Septemba 2022 katika ukumbi wa mikutano wa
Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma.
Dkt. Ndumbaro amesema ‘’ katika kauli mbiu yenu nimeona kuna
mambo kadhaa ikiwemo uzingztiwaji wa sheria, hivyo sisi Mawakili wa Serikali
tuhakikishe kwamba utekelezaji wa majukumu ya Serikali popote mlipo unazingatia
sheria kwa maendeleo ya Taifa’’.
Dkt Ndumbaro ameongeza kuwa Wizara inategemea kupitia Chama
cha Mawakili wa Serikali mchango mkubwa utapatikana katika sera, Katiba na haki
za binadamu kwani Serikali imekuwa ikishambuliwa sana katika maeneo hayo.
Amesisistiza, ‘’maeneo ya Katiba na Haki za Binadamu
yawekewe mkazo kutokana na hoja mbalimbali zinazoibuliwa na wananchi ikiwemo
mahitaji ya Katiba Mpya’’.
Vilevile, Dkt. Ndumbaro amemtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara Mawakili wa Serikali ili kuwajengea uwezo na
kuweza kuisaidia Serikali hasa katika maeneo ya Uendeshaji Mashtaka, Msaada wa
Kisheria na Maliasilia za nchi.
Aidha, Dkt. Ndumbaro amewaasa Mawakili wa Serikali
kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani vinawavunjia heshima na uaminifu kwenye
jamii katika kutenda kazi zao kutokana na watu wanaowapa rushwa kuwatangaza
kwenye jamii.
Zaidi ya Hayo, Dkt. Ndumbaro amewasisitiza Mawakili hao wa
Serikali kutunza siri za Serikali na kujikita kwenye matumizi ya TEHAMA
yanayozingatia sheria na weledi na kuepuka kutumia vibaya mitandao na kuchafua
sifa ya Serikali.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amewaasa viongozi wa muda walioteuliwa
na Chama cha Mawakili wa Serikali kuwa watiifu na kujitolea kwa moyo katika
kutenda kazi za chama hicho na pia kujiepusha na mambo ya kisiasa kwani chama
hicho sio cha kisiasa.
Comments
Post a Comment