RAIS SAMIA ASISITIZA ELIMU YA SHERIA KWA WANANCHI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongea katika  maadhimisho ya miaka 25 ya kuwepo kwa Taasisi ya WiLDAF tarehe 20 Oktoba, 2022 Jijini Dar es Salaam.                                                                                                                                                                    

Meza kuu


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuongea na wanannchi katika maadhimisho ya miaka 25 ya kuwepo kwa Taasisi ya WiLDAF tarehe 20 Oktoba, 2022 Jijini Dar es Salaam.                                                                                                            



Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Shertia Bi. Mary Makondo (wa tatu kulia) na waalikwa wengine wakimsikiliza Rais.
 XXXXXXXXXXXXXX

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesisitiza elimu ya sheria kuendelea kutolewa kwa wananchi ili kuwawezesha wananchi kujua sababu za sheria kutungwa, malengo ya sheria na adhabu zilizoko kwenye sheria husika.

Mhe. Rais ameyasema hayo alipokuwa akihutubia Taifa kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya kuwepo kwa Taasisi ya WiLDAF tarehe 20 Oktoba, 2022 Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais amesema “pamoja na sheria kuwepo lakini bado mambo ya ajabu ajabu yanatokea, hii inaonesha sheria peke yake haitoshi, Sheria hizi zinahitaji kutambulika na kukubaliwa. Wananchi hawawezi kuzitambua na kuzikubali hadi twende tuwaambie kuna sheria hii na ina vifungu hivi na hivi, lengo lake ni kukataza hili na hili na adhabu yake ni hii, hilo likifanyika hata sheria kandamizi za kimila zilizopo zitamezwa.” 

Vile vile Mhe. Rais ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kuanza kutunga sheria kwa lugha ya Kiswahili na kutafsiri zilizopo kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha yetu ya Kiswahili zoezi ambalo litarahisisha utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi.

Wakati mchakato wa mabadiliko ya sheria ya ndoa ukiendelea, Mhe. Rais amewaomba WiLDAF na Wadau wengine wa haki kuunga mkono sera ya Serikali ambayo imeweka elimu ya msingi hadi kidato cha sita bure. Sera hii inamfanya mtoto  kuongeza miaka akiwa shuleni kabla ya kufikiria kuoa au kuolewa na si aghalabu mzazi kuruhusu binti yake kuolewa angali shuleni.

Aidha, Mhe. Rais ameagiza kuangaliwa kwa sheria ambazo zinazorotesha sheria nzuri zilizowekwa, mfano sheria ya kimila ambayo haizingatii haki ya mwanamke kumiliki ardhi inazorotesha Sheria ya ardhi  ya mwaka 1999 iliyotungwa na Serikali.

“Ni jambo la kushangaza katika karne hii ya 21 mtu anasimama na anapinga mwanamke kurithi mali na ardhi aliyoacha mume wake kwani kwa kawaida baada ya baba kufariki anayetunza watoto ni mke na ni lazima awe na nyenzo za kutunza watoto,” alisema Mhe. Rais.

Mhe. Dkt Damas Ndumbaro Waziri wa Katiba na Sheria akimkaribisha Mhe. Rais amesema Wizara inaendelea kufanya mabadiliko ya mifumo ya utoaji haki hususan kumwondolea mwanamke kadhia ya kusumbuka muda mrefu kutafuta haki mahakamani na kwenye vyombo vingine vya kutoa haki. 

“Falsafa ya Wizara ni kufanya mfumo wa utoaji haki utoe haki kwa wakati na kwa gharama nafuu. Muda utakao okolewa utumike na mwananchi katika kuzalisha mali na kutunza familia. Mfumo wa utoaji haki uweze kuleta tahafifu kwa wanyonge hususan wanawake na watoto,” alisema Dkt. Ndumbaro.

Waziri Ndumbaro ameongeza kuwa ili kufanikisha azma hiyo Wizara yake imejikita katika matumizi ya TEHAMA, ametaja baadhi ya maeneo yanayotumia mifumo ya TEHAMA kuwa ni pamoja na Usajili wa watoa huduma za kisheria, usajili wa Wasuluhishi, Wapatanishi, Watoa huduma za Maridhiano na Mashauriano. Eneo lingine linalotumia TEHAMA ni upokeaji wa maombi ya msaada wa kisheria, maombi ya kuchukua wahalifu na kuwapeleka nje ya nchi na maombi ya kuongezewa muda wa kufungua mashauri.

Awali wakati akitoa salaam, Wakili Anna Kulaya Mratibu Kitaifa wa Shirika la WiLDAF ambalo moja ya malengo yake ni kuwawezesha wanawake kiuchumi amesema sheria ni nyenzo muhimu katika kuboresha maisha ya wanawake, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutunga na kuboresha sheria zinazolinda haki za wanawake nchini.

Katika maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na Viongozi wengine wa Serikali akiwemo Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, Bi. Mary Makondo Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Wanaharakati waanzilishi wa WiLDAF, Wanasheria, Mawakili, Wadau wa Maendeleo na waalikwa wengine yalikuwa na kauli mbiu isemayo “Miaka 25 ya kutumia sheria kuboresha Maisha ya wanawake.”

Bi. Kate Somvongsiri kutoka Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani ameipongeza Serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulinda haki za wanawake na wasichana katika kuondoa changamoto za usawa kijinsia.


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA