WADAU WA HAKI MTOTO WATAKIWA KUTOA TAARIFA NA TAKWIMU SAHIHI KUHUSU UKATILI DHIDI YA WATOTO


Mkurugenzi wa Kitengo cha Msaada wa kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Felistas Mushi akiongea na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa kikao cha siku mbili cha Jukwaa la Haki Mtoto kinachofanyika Oktoba 20 na 21,  jijini Arusha.
Washiriki wa kikao cha siku mbili cha Jukwaa la Haki Mtoto kinachofanyika Oktoba 20 na 21,  jijini Arusha.


Mwakilishi kutoka UNICEF Bi. Victoria Mgonela akiongea na washiriki wa kikao cha siku mbili cha Jukwaa la Haki Mtoto kinachofanyika Oktoba 20 na 21,  jijini Arusha.

Picha ya pamoja.
XXXXXXXXXXXXX

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amewataka wadau wa Haki Mtoto kujikita katika majukumu yao na kutoa taarifa na takwimu sahihi  dhidi ya ukatili wa watoto ili kuwezesha Serikali inapopanga afua iwe na taarifa na takwimu sahihi zitakazowezesha kupanga mikakati ambayo itasaidia kutokomeza au kupunguza vitendo hivyo vya ukatili.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Msaada wa kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Felistas Mushi kwa niaba ya Katibu Mkuu huyo katika ufunguzi wa kikao cha siku mbili cha Jukwaa la Haki Mtoto kinachofanyika Oktoba 20 na 21,  jijini Arusha.

Akisoma hotuba hiyo Bi. Felistas amesema "Katibu Mkuu amesisitiza maeneo matatu ya kuzingatia katika utekelezwaji wa Jukwaaa la Haki Mtoto ikiwemo kutolewa kwa Msaada wa Kisheria kwa wahanga wa masuala ya ukatili, elimu ya masuala ya sheria kutolewa kwa wananchi na uwasilishwaji wa taarifa au takwimu uzingatie suala zima la ukatili".

Ameongeza kuwa “Huduma ya Msaada wa kisheria iendelee kutolewa kwa kiwango cha kutosha kwa wahanga hususan watoto na kujenga uelewa kwa jamii katika masuala ya ukatili kwa upana zaidi’’

Kwa upande mwingine Bi. Felistas amesema Madawati ya kijinsia yamekuwa na tija sana kwa sababu waathirika wanaojua uwepo wa madawati haya wamekuwa wakiyatumia. Na kupitia madawati haya Umma umeweza kufahamu kwamba kuna vitendo vya ukatili ambavyo vinaongezeka.

Bi. Felistas ameongeza kuwa kwenye kikao kilichofanyika mwezi wa nne mwaka 2022 taarifa zilionyesha kwamba vitendo vya ukatili vinavyoongezeka ni ulawiti kwa watoto wa kiume na ubakaji kwa watoto wa kike na vitendo hivi vinafanywa na watu wa karibu.

Aidha, Mwakilishi kutoka UNICEF Bi. Victoria Mgonela amesema shirika lake litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na kupunguza mmomonyoko wa maadili ili kuweza kujenga nchi yenye uchumi imara. 

Naye Mratibu wa mtandao wa wasaidizi wa kisheria Tanzania (TAPANET) Bw. Tolbert Mmasy amesema mtandao huo ni muhimu kwani wamekuwa wakiibua ukatili wa watoto katika maeneo mbalimbali hata visa vinavyoripotiwa na vyombo vya habari vimeibuliwa na watoa huduma za msaada wa kisheria.

Aliongeza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la hivi visa ambapo changamoto kubwa ni mmomonyoko wa maadili, pia amesema watoto wanaosoma mbali na maeneo wanayoishi wamekuwa wakikumbwa sana na ukatili huu. 

Kikao hicho kimeshirikisha washiriki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi za Serikali ikiwemo Mahakama, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Asasi za Kiraia na Vyuo vikuu.

 


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA