KULINDA HAKI ZA BINADAMU NI KULETA USTAWI WA TAIFA: DKT. NDUMBARO





 XXXXXXXXXXXXX

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema nchi inapolinda haki za binadamu kwa mtu mmoja mmoja, makundi na jamii kwa ujumla kwa kuzingatia Katiba ya nchi kunaleta ustawi wa Taifa na maendeleo ya watu.

Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uelewa Maafisa Viungo wa Haki za Binadamu kutoka Wizara, Idara na Taasisi za Serikali juu ya mfumo wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu leo tarehe 1 Novemba, 2022 Jijini Arusha.

Katika hotuba yake Dkt. Ndumbaro amesema “Serikali itaendelea kuheshimu na kulinda misingi ya demokrasia na haki za binadamu kwa ajili ya ustawi wa Taifa kwa kuzingatia Katiba ya nchi na Serikali itachukua hatua za kuheshimu na kuzingatia mifumo ya kulinda haki za binadamu”

Aidha, Dkt. Ndumbaro amesisitiza kwamba kulindwa kwa haki za binadamu huwafanya wananchi waishi kwa amani na kuwawezesha kutekeleza malengo yao ya kimaisha na kupata maendeleo chanya.

Akiongelea lengo la mafunzo hayo Dkt. Ndumbaro amesema “lengo la mafunzo ya leo ni kuwajengea uwezo Maafisa Viungo wa Haki za Binadamu ili muweze kuungamanisha majukumu yenu ya kila siku ya haki za binadamu pamoja na mfumo wa Umoja wa Mataifa wa kufuatilia na kutoa taarifa zinazohusika na haki za binadamu katika maeneo yenu ya kazi.”

Akimalizia hotuba yake Dkt. Ndumbaro ameagiza kuwa baada ya mafunzo hayo Maafisa Viungo wa Haki za Binadamu wawe nguzo katika ufuatiliaji na utumaji wa taarifa sahihi na stahiki Wizarani.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Nkasori Sarakikya amesema Maafisa Viungo walioteuliwa wataimarisha mfumo wa mawasiliano kati ya Wizara na Taasisi wakati wa kuandaa taarifa za utekelezaji wa haki za binadamu.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Kanda ya Afrika Mashariki Bi. Meena Ramkaun ameipongeza Serikali kwa kusema ni manufaa makubwa kwa nchi kuwa na mfumo wa uratibu wa kitaifa wa kuripoti na ufuatiliaji wa taarifa za haki za binadamu.

 


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA