MALALAMIKO YA WANAFUNZI WA LAW SCHOOL HAYANA USHAHIDI


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (katikati) akipokea ripoti ya tathmini ya mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (law school) kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Harrison Mwakyembe. Anayeshuhudia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Mary Makondo.

Dkt. Ndumbaro akikabidhi ripoti kwa Katibu Mkuu Bi. Mary Makondo.


Dkt. Ndumbaro akikabidhi ripoti kwa Naibu Katibu Mkuu Dkt. Khatibu Kazungu.


Mwenyekiti wa Kamati Dkt. Harrison Mwakyembe (mwenye kofia) akielezea jambo.

Picha ya Viongozi wa wizara na Wajumbe wa Kamati.

XXXXXXXXXXXXXXXX

Kamati ya Tathmini ya Mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria Kwa Vitendo Tanzania yakosa ushahidi wa kuthibitisha tuhuma za rushwa, uonevu na upendeleo katika utungaji na usahihishaji wa mitihani zilizotolewa na wanafunzi wa kundi la 33.

Hayo yamebainishwa Leo Novemba 20, 2022 wakati Kamati hiyo ikikabidhi ripoti ya tathmini hiyo Kwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt Damas Ndumbaro, jijini Dar Es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kwa kuzingatia unyeti wa Taasisi na wajibu ilionao ambao unahitaji uadilifu, Kamati imewasilisha majina ya Wakufunzi waliotajwa katika tuhuma hizo kwa uongozi wa juu wa Taasisi ili uweze kufuatilia mienendo yao.

Vilevile, Kamati hiyo imepokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi wa Taasisi hiyo kuhusu zoezi la ukataji wa rufaa wanapokuwa hawakubaliani na matokeo, na kamati hiyo katika tathmini yake imegundua kwamba, utaratibu wa rufaa haujakaa vizuri kwani haumpi mlalamikaji kujua kwa uhakika msingi wa malalamiko yake.

Aidha, Kamati imebaini changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa Mahakama ya kufundishia, uchakavu wa miundombinu,  uwezo mdogo wa wanafunzi wanaojiunga na Taasisi hiyo, na vyuo vingi vya sheria kutozingatia uwiano wa walimu na wanafunzi.

Vilevile Kamati hiyo imeshauri Baraza la Elimu ya Sheria (CLE) ambalo ndilo lenye mamlaka ya kusimamia na kuishauri Serikali kuhusu elimu na taaluma ya sheria nchini liundiwe sekretarieti, kupewa ofisi na bajeti yake ili liweze kutekeleza majukumu yake yaliyoainishwa kisheria.

Naye, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Damas Ndumbaro ameishukuru Kamati hiyo kwa tathmini waliyoifanya na kuahidi kushughulikia yale yote yaliyobainishwa katika ripoti waliyokabidhi.

 


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA