WATUMISHI KATIBA NA SHERIA WATAKIWA KUCHAPA KAZI NA KUZINGATIA UADILIFU NA NIDHAMU
Viongozi waliowahi kuongoza katika wizara hiyo kwa nafasi mbalimbali wakikabidhiwa zawadi.
Watumishi wastaafu wakikabidhiwa zawadi.
Watumishi
wa Wizara ya Katiba na Sheria wametakiwa kuelewa majukumu waliyonayo si
lelemama hivyo wayatekeleze kwa kuzingatia uchapakazi, uadilifu, nidhamu na
kufanya kazi kama timu ili kuweza kuleta matokeo mazuri ya kazi zao.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro Novemba 3,
2022 jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na watumishi hao kabla ya
hafla ya kuwaaga viongozi na watumishi wa Wizara hiyo waliostaafu.
Waziri
Ndumbaro amesema ‘’Wizara hii ni wizara kubwa na nyeti kwa sababu imeshikilia
Katiba ya nchi, pia inashughulika na sheria ambayo ndiyo kila kitu katika
utawala wa nchi’’
Dkt.
Ndumbaro ameongeza kuwa ‘’Nataka muelewe kwamba jukumu tulilonalo si lelemama
tutaweza kulitekeleza tukizingatia uchapakazi, uadilifuna nidhamu na kufanya
kazi kama timu’’
Dkt.
Ndumbaro amesisitiza kuwa ni lazima watumishi wajitume, wawe na maadili na
nidhamu ya kazi na Wakuu wa Idara na Vitengo wajue uwezo wa watumishi wanaowasimamia
ili kujenga taswira mpya ya wizara.
Mbali
na hayo Dkt. Ndumbaro amewaasa watumishi hao kuwa ‘’wajibu wetu ni kuendelea
kushirikiana tuishi kama familia, nataka hii wizara iwe sehemu nzuri Zaidi ya
mtu kufanya kazi’’
Naye
Katibu Mkuu Bi. Mary Makondo amemhakikishia Waziri kuwa maelekezo yake
yamepokelewa na kumuahidi watumishi watafanya kazi kwa bidii na kuendelea kuwa
wabunifu ili kuleta matokeo chanya kwa wizara.
Bi.
Makondo amesema ‘’tukuahidi tumesikia maelekezo yako na tutaendelea kuwa
wabunifu, tuna jukumu kubwa la kuwajibikja ipasavyo na tutafanya kazi kwa
weledi’’.
Wakati
huohuo kwenye hafla ya kuwaaga viongozi na watumishi waliostaafu Dkt. Ndumbaro
aliwashukuru kwa utumishi na kuthamini mchango wao katika kipindi
walichotumikia wizara hii kwa kuwakabidhi zawadi mbalimbali kama ukumbusho kwao.
Viongozi
waliowahi kuongoza wizara hii na kuagwa jana ni pamoja na Mhe. George Simbachawene,
Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Prof. Sifuni Mchome na Bw. Amon mpanju.
Watumishi
wengine walioagwa ni Bw. Simbaufoo Swai, Bi. Diana Makule, Bi. Iluminata
Matindi na Bw. Amani Goha.
Comments
Post a Comment