HATUA KALI ZAIDI KUCHUKULIWA KWA WAHALIFU WA MAKOSA YA UNYANYASAJI KIJINSIA: DKT. NDUMBARO




XXXXXXXXXXXXXX

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema Serikali imejipanga kuchukua hatua kali zaidi kwa wahalifu wa makosa ya unyanyasaji kijinsia.

Waziri Ndumbaro ameyasema hayo wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST) Novemba 5, 2022 Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Ndumaro amesema “rai ya Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kupaza sauti siku zote 365 za mwaka kutambua viashiria vya unyanyasaji wa kijinsia na kuvitolea taarifa kwenye vyombo husika ili sheria ichukue mkondo wake.”

Katika hatua nyingine Mhe. Ndumbaro amesema “Wizara ya Katiba na Sheria iko mbioni kuanzisha usajili wa mtandaoni (online registry) kwa mtu ambaye amethibitishwa na Mahakama kuwa na hatia ya unyanyasaji wa kijinsia.” Watu watakaokuwa katika orodha hiyo hawatakuwa na uwezo wa kukopa benki wala kupata ajira, miongoni mwa huduma zingine.

Kwenye maadhimisho hayo, Sanaa, Vyombo vya Habari na Huduma za msaada wa Kisheria vilitumika kuelimisha jamii kupinga ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.

Aidha, Mhe. Geophrey Pinda Naibu Waziri wa Katiba na Sheria akimkaribisha Mgeni Rasmi amesema wakati umefika Wizara ya Katiba na Sheria kuwa na Dawati la msaada wa kisheria.

Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo akitoa salaam katika maadhimisho hayo amesema hatua zitaendelea kuchukuliwa kwa wahusika wa matukio ya ukatili wa kijinsia yanayoripotiwa. Bi Makondo amesema “Juhudi za Seriki ni kutokomeza ukatili wa kijinsia hivyo wananchi tuiunge mkono Serikali kwa kutoa taarifa za matukio hayo.”

Vile vile Bi. Kathrin Steinbrenner Naibu Balozi wa Ujerumani nchini amesema harakati za kupigania haki ni kwa makundi yote wanawake, watoto na wanaume kwani makundi yote yanapitia ukatili wa kijinsia. Amempongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika kutetea haki za binadamu ambapo Ujerumani inaungana na Tanzania katika vita ya kupinga ukatili wa kijinsia. 

Akitoa salaam za ukaribisho, Jaji Dkt. Benhaji Masoud Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo amesema ukatili na unyanyasaji wa kijinsia si tu una athari kwa wahusika bali pia unaathiri maendeleo ya Taifa. Amesema Taasisi yake iko tayari kupambana na vita vya ukatili wa kijinsia ili kuwa na jamii salama na yenye maendeleo.

 

 



 


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA