MAONESHO YA WIKI YA SHERIA: WATATUZI WA MIGOGORO KWA NJIA MBADALA WAANZA KUSAJILIWA KIELEKTRONIKI.

 




Wizara ya Katiba na Sheria imeanza kuwasajili watatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, upatanishi, majadiliano na ufanyaji maridhiano kwa kupitia mfumo wa kielektroniki ulioundwa mwaka jana na kuanza kutumika rasmi Juni, 2022 kwa lengo la kurahisisha hatua zinazotakiwa kutekelezwa wakati wa usajili.

Taarifa hiyo imetolewa na Wakili wa Serikali Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bwana  Elia Athanas alipokuwa anamwelezea Mgeni Rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria kabla ya uzinduzi rasmi wa maonesho haya ya Wiki ya Sheria.

Wakili Athanas alisema mfumo huu umekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wanaojihusisha na kazi za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala kwani hivi sasa hawalazimiki tena kusafiri hadi Dodoma kwa ajili ya kuwasilisha maombi yao ya usajili  bali kwa kutumia kompyuta yenye internet wanaweza kutuma nyaraka na kuwasilisha maombi yao.

“Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo huu, mwanachi alilazimika kuja wizarani kupata maelezo na kuleta nyaraka yeye mwenyewe, mfumo huu wa kielektroniki ulioanza kutumika Juni 2022, unamuwezesha mtu yeyote mahali alipo ambaye anajihusisha mambo ya utatuzi wa migogoro kuingia katika mtandao ambao utamuelekeza hatua zote za kujisali ikiwemo kuwasilisha nyaraka zote muhimu kwa ajili ya kukamilisha usajili” Alisema Wakili Athanas.

Akielezea jinsi ya kukamilisha usajili, wakili Athanas alisema mara baada ya nyaraka zote zilizohitajika kuwasilishwa, hatua inayofuata ni jopo la ithibati kupitia ombi hilo na likiridhia, cheti huandaliwa na mwombaji atapata cheti chake kupitia mfumo huohuo.

“Toka kuanza kutumika kwa mfumo huu, tumefanikiwa kuwasajili watatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, upatanishi, majadiliano na ufanyaji maridhiano 494 ambao waliwasilisha maombi yao na baada ya jopo la ithibati kuthibitisha wakapata vyeti”. Aliongeza Wakili huyo.

Mwaka 2020, Serikali ilipitisha Sheria ya Usuluhishi iliyoweka mfumo wa uratibu wa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala ambapo mwananchi au taasisi binafsi inayotaka kufanya kazi za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala ikiwemo wapatanishi, wafanya maridhiano na majadiliano wanapaswa kusajiliwa na Msajili aliyepo chini ya Wizara ya katiba na sheria ili waweze kutambulika rasmi.

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA