KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YAELEKEZA LUGHA ZA KIINGEREZA NA KISWAHILI KUTUMIKA WAKATI WA UTUNGAJI WA SHERIA.
Sehemu ya wanakamati wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria na Viongozi wa Taasisi za Wizara hiyo wakifuatilia aarifa ya Mhe. Waziri Ndumbaro.
Na George Mwakyembe & Lusajo Mwakabuku – WKS.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeielekeza Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutumia lugha zote mbili wakati wa utungaji wa
Sheria na kanuni yaani Kiingereza na Kiswahili ili kuepusha kazi hiyo kufanywa
mara mbili kunakopelekea kuongezeka kwa gharama rasilimali fedha na muda pale
Sheria husika inapotakiwa kutafsiriwa baada ya kupitishwa.
Maelekezo hayo yametolewa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala, Katiba na Sheria walipokuwa wakipokea taarifa inayohusu Muundo na
Majukumu ya Wizara pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria
iliyowasilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro, 12 Machi,
2023.
Akiwasilisha taarifa mbele ya Kamati hiyo, Waziri Ndumbaro akiwa
ameambatana na Menejimenti ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zote zilicho
chini ya Wizara ya Katiba na Sheria amesema Wizara ya Katiba na Sheria imekuwa
na mchango mkubwa katika kuhakikisha inasimamia ipasavyo suala la haki na usawa
jambo linalopelekea wawekezaji kuvutiwa kuwekeza nchini.
"Wizara ya Katiba na Sheria ni Wizara inayochangia kwa kiasi
kikubwa katika kuvutia wawekezaji kwa kuimarisha Haki na Usawa, wawekezaji
hawawezi kuja kuwekeza nchini kama hakuna Haki na Usawa”. Alisema Mhe.
Ndumbaro.
Akichangia kwenye kikao hicho Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mh. Jaji Dkt
Eliezer Feleshi amesema jukumu kubwa lililopo sasa ni kuendelea kutafsiri
Sheria zote 446 pamoja na Sheria ndogo 29,172 na tayari Wizara ilishajipanga na
wanaendelea na kazi hiyo, maelezo haya yalipelekea wajumbe kutaka utungaji wa
Sheria hizo ufanyike katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili ili kuepusha kazi
ya kutafsiri baada ya mswada wa Sheria kupitishwa.
Pamoja na jukumu hilo Jaji Dkt Feleshi amesema ofisi yake pia ina jukumu
la kusimamia majadiliano ya migogoro mbalimbali iliyopo Mahakamani ili migogoro
hiyo iijadiliwe nje ya Mahakama kama Kauli Mbiu ya Wiki ya Sheria iliyofanyika
February mwaka huu iliyoelekeza umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya
usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof, Elisante Ole Gabriel ameishukuru
Wizara kwa Ushirikiano wanaowapa na kusema sasa wamejipanga kuboresha Mahakama
za Kata nchi mzima kuhakisha kuwa zinakuwa na miundo mbinu bora na ya kisasa.
Katika hatua nyingine, Kamati imeelekeza kuendelea kukiimarisha Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto kwani ni moja kati ya vyuo vinavyoipa sifa nchi
katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa Chuo bora chenye kuendeleza
watumishi wa Mahakama. Kamati vile vile imeelekeza Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora ambacho ni chombo cha Kikatiba chenye jukumu la kuhakikisha
kinalinda haki za binadamu hususan masuala ya makundi maalumu ya wanawake na
watoto kutekeleza majukumu yake ipasavyo hasa matukio mbalimbali ya ukiukwaji
wa haki za binadamu na watu yanapojitokeza badala ya kukaa kimya.
Baada ya wasilisho na maelekezo ya kamati, Mhe. Dkt. Ndumbaro alisema
kuwa Wizara yake imepokea maelekezo yote na akaiomba kamati kuwa utakapofika
wakati wa kuwasilisha Bajeti ya Wizara na Taasisi zake mbele ya Bunge, kamati
iiunge mkono ili bajeti itakayoombwa iweze kupitishwa na hivyo kuiwezesha
Wizara na Taasisi zake kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Comments
Post a Comment