DKT NDUMBARO AZINDUA KANUNI ZA WATOA TAARIFA


 Waziri wa Katiba na Sheria  Dkt. Damas Ndumbaro  akizindua  Kanuni za Watoa Taarifa  na Ulinzi  wa Mashahidi,  tarehe  28 Februari 2023, Kulia Naibu Waziri Pauline Gekul  na  Kushoto Naibu Katibu Mkuu Khatibu Kazungu. 


                               xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx


Na Mwandishi wetu, Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt Damas Ndumbaro amezindua Kanuni za Watoa Taarifa na Ulinzi wa Mashahidi za mwaka 2023 na kueleza kuwa Kanuni hizo zitasaidia kufichua uhalifu na kuimarisha utoaji haki jinai.

Dkt Ndumbaro ameyasema hayo wakati wa kuzindua Kanuni hizo hatua ambayo inaashiria kuanza utekelezaji wa Sheria ya Watoa Taaarifa na Ulinzi wa Mashahidi ya mwaka 2016.

Katika uzinduzi huo ambao umefanyika tarehe 28 Februari, 2023 Dkt Ndumbaro amesema kanuni hizo zinaenda kusaidia uimarishaji utoaji wa haki jinai kwa sababu zinahusu utoaji wa taarifa za ukiukwaji wa sheria mbalimbali, makosa ya jinai, wizi wa mali za umma na ufisadi.

“Watoa taarifa hizi ni muhimu sana kwenye jamii, wanatwambia mali ya umma inaibiwa, katika historia ya nchi hii watoa taarifa wamesaidia kufukua mambo mengi yenye maslahi kwa jamii lakini walikuwa hawatambuliki kisheria.”

Aidha, Dkt Ndumbaro alisema sehemu ya pili ya kanuni hizo ni ulinzi wa mashahidi na kuwa ni eneo ambalo lilikuwa limelegalega hasa kwenye mfumo wa haki jinai.

“Kuna wakati mashahidi walikuwa wanaogopa kwenda kutoa ushahidi akihofia madhara ya yeye kutoa ushahidi.” Dkt Ndumbaro alisema uwepo wa sheria na kanuni hizo zinabeba mambo makuu matatu ambayo ni utawala bora, utoaji wa haki jinai na zinakoleza vita ya mapambano dhidi ya uhalifu.

“Tunaamini uzinduaji wa kanuni hizi unaenda kuwa chachu ya watu kuibua makosa mengi zaidi yanayofanyika kwasababu wanakinga kisheria na kanuni.”

 Vilevile, Dk Ndumbaro ameagiza kufanyika kwa mafunzo na utoaji elimu kwa watanzania na kusisitiza kuwa sheria hiyo ikitumika vizuri mali za umma zitaokolewa.

“Wale wadokozi wadokozi, arobaini zao zimefika kwa sheria na kanuni hizi, inakwenda kulinda uchumi wa nchini na kuwaumbua na kuwaanika wahalifu na kwenda kupunguza uhalifu unaowaathiri sana wananchi.”

Pia Dkt Ndumbaro amezitaka mamlaka zinazopaswa kupokea taarifa hizo za uhalifu kuhakikisha  zinafika  kwenye vyombo vya dola ambavyo navyo vinatakiwa kutekeleza kwa haraka, hatua itakayoongeza imani kwa watoa taarifa.

Dkt Ndumbaro alisema pia kanuni hizo zitavisaidia vyombo vya habari ambavyo navyo vimekuwa vikipokea taarifa kutoka kwa watoa taarifa na hapo nyuma ulinzi ulikuwa ni maadili na sasa vitakuwa na kinga ya kisheria.

 

Naye Naibu Katibu Mkuu, Dkt Khatib Kazungu alisema watoa taarifa na mashahidi ni watu muhimu katika mnyororo wa haki jinai kwani taarifa wanazozitoa zinawezesha kufichua uhalifu kwenye jamii, na mashahidi wamekuwa wakiongeza ufanisi katika uendeshaji wa mashauri ya jinai kwa wakati.

 “Uwepo wa kanuni hizi utawezesha wananchi kujisikia huru, kutoa taarifa zozote za uhalifu uliofanyika au unaopangwa kufanyika na pia utawafanya mashahidi kuwa huru kutoa ushahidi mahakamini kwani zinawahakikishia ulinzi hatua ambayo itasaidia kuongeza imani.”

Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki, Kharist Luanda alisema kanuni hizo zinaweka mfumo wa kisheria wa kuwatambua, kuwalinda, kuwalipa fidia na kuwapatia zawadi watoa taarifa na mashahidi kulingana na taratibu na vigezo vilivyowekwa kwenye kanuni. 

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA