Ndumbaro awataka watumishi wa Serikali kuwa wabunifu.


 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akihutubia kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, tarehe 24 Aprili, 2023 Jijini Dodoma.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx


Na William Mabusi

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewataka watumishi kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wawe wabunifu katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ili kuleta tija katika utendaji kazi.

Mhe. Ndumbaro ameyasema hayo wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa kikao cha Baraza la wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, tarehe 24 Aprili, 2023 Jijini Dodoma.

“Fanyeni kazi kwa kujituma na kuwa wabunifu, miundo na mifumo iliyopo sasa ilibuniwa na watu na kila baada ya muda inatakiwa kufanyiwa mapitio na hilo litawezekana kama kuna ubunifu.” Alisema Dkt. Ndumbaro.

Aidha, Dkt. Ndumbaro amewaasa wajumbe wa Baraza kutumia kikao hicho, kwanza kujadili utekelezaji wa mpango wa bajeti wa mwaka wa fedha 2022/23 mafanikio, changamoto na ufumbuzi wake, pili kujadili mpango wa bajeti ya Tume kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Vikao vya Mabaraza ya wafanyakazi ni matakwa ya kisheria ambapo kupitia mabaraza wafanyakazi hushirikishwa katika masuala ya maamuzi mahala pao pa kazi. Lengo likiwa kujenga umoja, kuondoa majungu, kuondoa migogoro mahali pa kazi ili kuleta utendaji wenye tija.

Awali, akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema ujenzi wa jengo la sakafu sita la ofisi za Tume ya Mahakama jijini Dodoma unakwenda vizuri na inategemewa kwamba watumishi wote wa Tume kuhamia Dodoma mwishoni mwa mwezi Julai, 2023 baada ya jengo kuwa limekamilika.

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA