Waziri Ndumbaro Asisitiza Utafiti wa Kisheria Kabla ya Sheria Kutungwa

 

Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akihutubia katika Kongamano la Tathmini ya Utekelezaji wa Sheria za Makosa dhidi ya Maadili ya Tanzania, lilioandaliwa na Tume ya kurekebisha sheria Tanzania, tarehe 05 Aprili, 2023 Jijini Dodoma.

                                                             xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

William Mabusi na Lusajo Mwakabuku - WKS

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesisitiza kufanya kwa utafiti wa kisheria kabla ya kutungwa kwa sheria ili sheria zitakazotungwa baada ya tafiti zitumike kwa muda mrefu kabla ya kufanyiwa marekebisho.

Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo wakati alipofungua Kongamano la Tathmini ya Utekelezaji wa Sheria za Makosa dhidi ya Maadili ya Tanzania, lilioandaliwa na Tume ya kurekebisha sheria Tanzania, tarehe 05 Aprili, 2023 Jijini Dodoma.

“Kukosekana kwa utafiti wa kisheria hupelekea mabadiliko ya mara kwa mara ya sheria. Hivyo kabla ya sheria kutungwa utangulie utafiti wa kisheria. Sheria zikitungwa baada ya kufanyiwa utafiti hudumu kwa muda mrefu kabla ya kufikiriwa kufanyiwa marekebisho.” Alisema Dkt. Ndumbaro.

Aidha, Dkt. Ndumbaro ameagiza Tume kuendelea kutoa elimu ya sheria ambapo hadi sasa Tanzania ina jumla sheria 447, “Sheria hizi ni nyingi na wananchi hawatazijua pasipokuwepo na mkakati wa kutoa elimu kwa umma. Na kwa kuzingatia hilo moja ya vipaumbele vya Wizara ya Katiba na Sheria katika Bajeti yake ya mwaka 2023/24 ni kutoa elimu ya sheria na Katiba kwa Watanzania.”

Kongamano hili limekuja wakati mwafaka kwani kumekuwepo na ongezeko la vilio kuhusu unyanyasaji mkubwa wa kijinsia na kingono katika jamaii. Maoni yatakayotolewa na washiriki katika Kongamano hilo yatasaidia kupaza sauti katika kukabiliana na mmomonyoko wa maadili nchini.

Kwa kuwa Asasi za Kiraia na Wadau wa haki wamekuwa washirika muhimu wakisaidiana na Serikali kukemea ukiukwaji wa haki za binadamu, Dkt. Ndumbaro ametoa wito kwa Wadau kuandaa makongamano kama haya ili elimu na maoni mengi yazidi kutolewa kwa wananchi kuhusu sheria na hivyo kujua haki zao.

Awali akitoa salaam katika Kongamano hilo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bw. Griffin Mwakapeje amesema lengo la Kongamano hilo ni Tume kupata maoni ya kuwezesha kutimiza majukumu yake ya Kufanya mapitio ya sheria, Kurekebisha sheria, Kufanya maboresho ya sheria katika kulinda na kukuza maadili kwenye jamii ya Taifa letu.


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA