SHINYANGA BADO YAANDAMWA NA UKATILI WA KIJINSIA
Afisa Ustawi wa Jamii wa Hospital ya Mkoa wa Shinyanga ambaye ni mmoja wa watalaam wanaotekeleza Mama Samia Legal Aid Campain( MSLAC ) Mkoani Shinyanga bwana Leopold Hamza akizungumza na wananchi .
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Lusajo Mwakabuku – WKS Shinyanga
Mkoa wa
Shinyanga umetajwa kuendelea kukabiliwa na matukio ya ukatili wa kijinsia
ikiwemo vipigo, mimba na mauaji na sababu kuu ikitajwa kuwa ni jamii kuendelea
kushikilia mila na desturi zilizopitwa na wakati, elimu ndogo pamoja na jamii
kutokuwa tayari kutoa taarifa ya matukio hayo.
Afisa Ustawi
wa Jamii wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ambaye ni mmoja wa wataalam
wanaoetekeleza Mama Samia Legal Aid Campaign (MSLAC) mkoani humo, bwana Leopold
Hamza aliyasema hayo wakati akitoa elimu ya kijinsia wakati timu hiyo ya
wataalam ilipokutana na wananchi wa vijiji vya Mwamagunguli na Galamba vya kata
ya Kolandoto mkoani Shinyanga ambapo mada mbalimbali za kisheria pamoja na
msaada wa kisheria vilitolewa kwa wananchi hao tarehe 14/06/2023.
Afisa Ustawi
wa Jamii huyo alisema bado changamoto za ukatili ni tatizo ikiwemo ukatili wa
utumikishwaji wa watoto katika shughuli mbalimbali zikiwemo katika mashamba ya
tumbaku, migodi midogo na majumbani, masuala ya ubakaji na ulawiti, mimba za
utotoni zinazokatisha ndoto za watoto pasipo kujali sheria ya mtoto ya mwaka
2009 na ile ya ajira.
“Kinachosikitisha
zaidi ni kwamba jamii inawafahamu wakosaji na mara nyingine kuwalinda kwa
kuamua kumalizia kesi nyumbani au kutotoa taarifa mapema wanapoona vitendo vya
ukatili. Hali hii hutoa mwanya kwa watuhumiwa kurudia vitendo hivyo mpaka siku
inayopelekea kifo. Hii inarudisha nyuma maendeleo ya nchi na juhudi za
Serikali katika kuleta maendeleo na kufikia usawa wa kijinsia na maendeleo
endelevu” Alisema bwana Leopold.
“Ndugu zangu
wa Kolandoto tupaze sauti unapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia au kuona
mtu akifanya vitendo hivyo basi chukua hatua kwa kuripoti tukio katika madawati
ya Polisi ya kijinsia vilevile unaweza kutoa taarifa ya tukio katika ofisi za
Ustawi wa Jamii, Serikali za Mitaa, Vituo vya afya, Vituo vya msaada wa
kisheria ili kupata huduma kwa wakati, msaidie mwathirika kuripoti tukio lake
ndipo tunaweza kutokomeza vitendo hivi.” Aliongeza bwana Leopold.
Naye mratibu
wa timu hiyo ya wataalam kutoka Wizara ya Katiba na Sheria bwana George Mollel
ambaye ni Wakili wa Serikali alitoa mada kuhusu haki za Watoto. Alieleza kuwa
mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka kumi na nane na haki za mtoto
zinajumuisha haki ya kushirikiana na wazazi wote wawili, kutambuliwa kibinadamu
na kupatiwa mahitaji ya msingi ya ulinzi wa mwili, chakula, elimu, huduma ya
afya, huku akifafanua sheria zinazofaa kwa ukuaji wa mtoto, haki za kiraia za
mtoto, uhuru wa kutokubaguliwa kutokana na jinsia, ulemavu, dini, kabila au
sifa nyingine.
Wakili
Mollel aliongeza kuwa ulinzi na usalama wa mtoto sio jukumu la Maafisa wa
ustawi wa jamii peke yao bali ni jukumu la Taifa kwa ujumla na kwamba hakuna
anayeruhusiwa kumdhuru, kumuumiza au kumnyonya mtoto. Yeyote anayejua kwamba
kuna mtoto anayeonewa au kutendewa vibaya hana budi kutoa taarifa kuhusu
vitendo hivyo kwa; Ustawi wa jamii, Polisi - Dawati la jinsia na Watoto, ofisi
za Serikali za Mtaa, Taasisi na Mashirika ya kijamii pamoja na kupiga simu
namba 116 ya kitaifa isiyo na tozo kwa lengo la kumlinda mtoto.
Aidha bwana
Mollea aliwasisitiza wale wote ambao wana changamoto binafsi na wamekosa nafasi
au hawako huru kueleza changamoto zao katika mikutano hiyo, kufika katika
mabanda yanayotoa huduma za kisheria mjini Shinyanga ambapo wataalam wapo hapo
wakitoa huduma hadi tarehe 21 Juni mwaka huu.
Wakitoa
salaamu za kuhitimisha mikutano hiyo kwa nyakati tofauti Wenyeviti wa vijiji
hivyo vya Mwamagunguli na Galamba vya Kata ya Kolandoto walimshukuru Mhe. Rais
kwa kuwaletea kampeni hii huku wakieleza kuwa katika vijiji vyao, ukatili wa
kijinsia licha ya kwamba bado upo lakini umepungua baada ya wananchi
kuelimishwa kupitia mikutano ya vijiji, ikiwemo wanandoa kutelekeza familia na
wanafunzi kuachishwa shule. Na hili limetokana na mikakati iliyowekwa na
Serikali katika kutoa elimu pamoja na kuwaonesha wananchi ni wapi pa kupeleka
malalamiko na kesi zao zinazohusu ukatili wa kijinsia katika jamii, kazi ambayo
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inaendelea kuifanya hivi sasa.
Mama Samia Legal Aid Kampeni inayoongozwa na kauli mbiu
inayosema ”Msaada wa kisheria kwa haki, usawa, amani na maendeleo” imedhamiria
kuongeza wigo wa ufikiwaji haki kwa wananchi, hususan walio vijijini na
ambao hawawezi kumudu gharama za Mawakili. Kampeni hii pia imekuwa msingi mzuri
wa kujenga uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za kikatiba na kisheria; jambo
ambalo ni muhimu katika kulinda na kukuza haki za binadamu nchini. Hii ni
kampeni ya miaka mitatu yenye lengo la kufikia mikoa yote nchini huku
ikitarajiwa kuhitimishwa mwaka 2026.
Comments
Post a Comment