SHINYANGA YAAHIDI USHIRIKIANO KATIKA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi, Christina Mdeme akiongea na Wananchi (Hawapo Pichani ) wakati wa uzinduzi wa Mama Samia Legal Aid Campain Mkoa wa Shinyanga , tarehe 11 Juni 2023.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Lusajo
Mwakabuku & William Mabusi – WKS Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme
ameiahidi Wizara ya Katiba na Sheria na wadau inaoshirikiana nao katika
kuendesha kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria - Mama Samia Legal Aid
Campaign kutoa ushirikiano wa hali na mali katika kufikia malengo ya kampeni
hii ya kutoa msaada wa kisheria kwa watanzania wote hasa wale waishio maeneo ya
pembezoni huku akiagiza kata zote zihakikishe zinanatenga maeneo maalum ambayo
watoa huduma wataweza kuongea na mwananchi mmoja mmoja kwa faragha.
Mheshimiwa Mndeme alitoa kauli hiyo alipokuwa
akihutubia kabla ya kuzindua rasmi utekelezaji wa kampeni hiyo mkoani Shinyanga
hafla iliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba Shinyanga mjini leo tarehe
11/06/2023 huku akiwaalika wakazi wote wa mkoa wa Shinyanga kushiriki Mama
Samia Legal Aid Campaign itakayotolewa bure kwa wanachi katika Halmashauri zote
sita kuanzia tarehe 11 - 21 Juni, 2023.
“Kwa mara nyingine tena, ninatoa wito kwamba sisi sote
tushikamane katika kumuunga mkono Kiongozi wetu, Mama yetu, Mlezi wetu na Mtetezi
wa Wananchi hususan wanyonge Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania katika kuondoa kadhia na viashiria vyote vya kuminya
upatikanaji wa haki hususan ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto ambayo
ndiyo changamoto kubwa ya Mkoa wa Shinyanga”. Alisema Mhe. Mndeme
Mkuu wa Mkoa huyo aliongeza kuwa kampeni hii
inatukumbusha watanzania wote uwajibikaji na usimamizi wa maamuzi yenye kuleta
haki na akatumia fursa hiyo kuwambusha watumishi wote kutojihusisha na masuala
ya rushwa inayopelekea kuzorotesha upatikanaji haki. Aidha Mhe. Mndeme
alimuahidi Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa katika
utekelezwaji wa Kampeni hii kwa kipindi cha miaka mitatu, ofisi yake itasimamia
maadili kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa haki kwa usawa.
Akitoa salaam na kumkaribisha Mgeni Rasmi, Naibu Waziri
wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amesema Wizara itaendelea
kushirikiana na Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kuhakikisha Kampeni
hiyo inatekelezwa ipasavyo ili kuwafikia watanzania kwenye Kata na Mitaa yote
nchini.
Mhe. Gekul amesema Wizara ya Katiba na Sheria
inamshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kudumisha utawala wa sheria; uzingatiwaji
wa haki za binadamu na watu na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wote
lakini kwa jicho la kipekee kwa wananchi wasiokuwa na uwezo.
“Huduma ya msaada wa kisheria kuwafikia wananchi bure
ni mapenzi na upendo mkubwa wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mwananchi
wa hali ya chini,” alisema Mhe. Gekul.
Akitoa maelezo ya awali kuhusu Mama Samia Legal Aid
Campaign, Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo ametaja mafanikio ya
kampeni hii toka ilipozinduliwa Mkoani Dodoma na kuendelea katika mkoa wa
Manyara kuwa ni pamoja na kusuluhishwa kwa migogoro mingi ya kijamii na hata
kifamilia iliyohusu ardhi iliyodumu miaka minne, mitano, na mwingine miaka kumi
kulikopelekea watu hawa ambao walikuwa hawasalimiani na hata hawazikani
kumaliza tofauti zao.
“Ziko familia ambazo wanafamilia walikuwa hawaongei
kutokana na migogoro inayohusiana na ardhi, mirathi na sasa wamesuluhishwa
katika Kampeni na wameungana katika kujenga familia zao na taifa kwa ujumla.”
alisema Bi. Makondo.
Aidha Bi. Makondo amesema kwa kuwa kuna uwezekano
mazingira ya mikoa hiyo kuwa sawa na Shinyanga hivyo uzoefu wa utatuzi wa
migogoro hiyo utasaidia Kampeni hiyo kushughulikia masuala yote ya ukatili wa
kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi na wosia na kuelimisha jamii kuhusu haki
na wajibu wao wa kisheria na kikatiba kwa mbinu na uzoefu uliopatikana mikoa
iliyotangulia na hivyo kuwezesha kampeni hiyo kufanyika kwa mafanikio makubwa
zaidi katika mkoa wa Shinyanga.
Umuhimu wa kampeni hii ni wa kipekee katika kuongeza
wigo wa ufikiwaji haki kwa wananchi, hususan walio vijijini na ambao
hawawezi kumudu gharama za mawakili. Kampeni hii pia imekuwa msingi mzuri wa
kujenga uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za kikatiba na kisheria; jambo
ambalo ni muhimu katika kulinda na kukuza haki za binadamu nchini. Hii ni
kampeni ya miaka mitatu yenye lengo la kufikia mikoa yote nchini huku
ikitarajiwa kuhitimishwa mwaka 2026.
Comments
Post a Comment