TULISTAHILI ELIMU HII: WAKAZI WA SALAWE
Wakili wa Kujitegemea Ndg. Chrisatus Chegula akitoa elimu ya sheria kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Salawe Halmashauri ya Shinyanga tarehe 16 Juni, 2023
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na William Mabusi – WKS Shinyanga
Wananchi wa
Kata ya Salawe na Solwa wamesema walistahili kupata elimu ya sheria na kupatiwa
huduma ya msaada wa kisheria kutokana na kuishi bila kujua sheria inasemaje
kwenye maeneo mengi na kutokujua wapi wapeleke mashauri yao hasa ya ardhi baada
ya kutofautiana na maamuzi ya mamlaka za chini na kutokujua namna ya
kushughulikia kero za wasimamizi wa mirathi.
Mikutano
katika Kata hizo mbili imefanyika kwa nyakati tofauti tarehe 16 Juni, 2023
ikiwa ni utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Sheria (MSLAC) katika
Halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga.
Bwana Heleman
Mathias Sanane wa kijiji cha Mwanga Songambele kutoka Kata ya Salawe
ameishukuru elimu ya sheria inayotolewa kwenye Kampeni hiyo kwa kusema
"wananchi wengi tumevaa miwani ya mbao yaani mtu alikuwa anakabidhiwa
usimamizi wa mirathi halafu anasema ng`ombe wote wa marehemu lete
hapa, mashamba yote ya marehemu yako chini yangu. Yaani watu tumepoteza haki
zetu kwa kutokujua sheria na ukijifanya kuhoji unatishiwa na kutakiwa kukaa
kimya.”
Naye ndugu
Bisanana Batemi mkazi wa Solwa amesema “elimu inayotolewa ni uhitaji wa kila
mtu na hasa wananchi wa vijijini ambao hatuna uelewa mkubwa wa sheria na
mabadiliko yake, sasa tumeelewa faida za kumiliki ardhi kisheria na jinsi ya
kugawana mali za ndoa.” akalinganisha utamu wa elimu ya sheria
iliyotolewa kama asali.
Akitoa mada
katika mikutano hiyo Wakili wa kujitegemea Bw. Chrisatus Chengula kutoka Chama
cha Mawakili Tanganyika ameyataja mambo ya kuzingatia wakati ardhi inahamishwa
kutoka kwa mmiliki mmoja kwenda kwa mwingine kuwa ni pamoja na mauziano hayo
kuwekwa kwenye maandishi na yasainiwe mbele ya mamlaka ya Serikali ya eneo
husika endapo hakuna Mwanasheria eneo hilo.
Kuhusu ardhi anayomilikishwa
mtu kama zawadi au urithi, mmiliki ahakikishe anaomba hati ya maandishi ya
zawadi ambayo itatumika kama kumbukumbu na itatumika wakati wa kuomba
kuthibitishwa umiliki wa eneo husika kisheria.
Wakili huyo
alisema msimamizi wa mirathi ambaye anaenda kinyume na taratibu za kisheria,
familia ina wajibu kisheria kwenda mahakamani na kuomba kutengua usimamizi
wake. Kwa kuwa mashauri ya mirathi hayana ukomo wananchi ambao hawajafungua
mirathi waliombwa kufungua mirathi ili kuepusha migogoro mingi inayotokea
katika familia baada ya mzazi au wazazi wote kufariki dunia.
Aidha, ilielezwa
kwamba Mamlaka ya chini kabisa katika kushughulikia mgogoro wa ardhi ni
Mabaraza ya Kata. Kabla ya mwaka 2021 Mabaraza hayo yalikuwa na mamlaka
kimahakama ya kutoa uamuzi lakini kuanzia 2021 sheria hiyo ilibadilishwa na
sasa Mabaraza hayo yanatakiwa kusuluhisha tu mgogoro wa ardhi. Endapo mgogoro
huo ukishindikana Baraza huandika hati ya kushindwa kusuluhisha mgogoro husika
na hati hiyo kupelekwa Baraza la Nyumba na Ardhi la Wilaya. Endapo mlalamikaji
hataridhika na uamuzi wa Baraza la Wilaya atakata rufaa kwenda Mahakama Kuu,
Kama bado hataridhika ataenda Mahakama ya Rufaa.
Comments
Post a Comment