WAHARIRI WAPEWA MAFUNZO YA SHERIA NA KANUNI ZA ULINZI KWA WATOA TAARIFA NA MASHAHIDI
Mkurugenzi wa Idara ya Katiba n Sheria Ndg. Khalist Luanda ambaye ndiye mwezeshaji wa mafunzo haya akitoa wasilisho kwa wahariri na wanahabari wandamizi walioshiriki mafunzo hayo 24.Juni 2023. Singida
Jesse Kwayu Mhariri mwandamizi akiuliza swali katika kikao cha mafunzo yaliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria Jukwaa la wahariri singinda leo tarehe 24Juni 2023.
Sehemu ya Wahariri na waandishi waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya habari na watumishi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria wakiendelea na mafunzo mjini Singida .
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na Lusajo Mwakabuku – WKS Singida
Wizara ya
Katiba na Sheria imefanya mafunzo kwa Wahariri na Wanahabari Waandamizi wa
Vyombo mbalimbali vya Habari juu ya Sheria ya kuwalinda Watoa Taarifa za
Uhalifu na Ulinzi wa Mashahidi, Sura ya 446 (The Whistleblower and Witness
Protection Act, Cap 446) kwa lengo la kuimarisha utawala bora na mapambano
dhidi ya uhalifu nchini.
Akiifafanua
sheria hiyo wakati akifanya wasilisho kwa Wanahabari tarehe 24/06/2023 mkoani
Singida, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki kutoka Wizara ya
Katiba na Sheria Bw. Khalist Luanda alisema Sheria inalenga kuhimiza na
kuwezesha utoaji taarifa za makosa ya kupanga, makosa ya rushwa, mienendo isiyo
ya maadili, matumizi mabaya ya ofisi, matendo hatarishi na ya ukiukaji wa
sheria.
Aidha Bw.
Luanda aliongeza kuwa sheria hiyo pia inalenga kutoa ulinzi wa watoa taarifa na
mashahidi dhidi ya matendo ya kulipiza kisasi na kuweka mfumo wa kutoa zawadi
na fidia kwa watoa taarifa na mashahidi ambao taarifa zao zitasaidia kukomeshwa
ama kuzuiwa kwa matukio ya uhalifu.
Mwezeshaji
Bw. Luanda aliwaeleza Wahariri masuala mbalimbali ya uhalifu ambayo mtu anaweza
kutoa taarifa kwa maslahi ya umma na sehemu ambazo mtoa taarifa anaweza kutoa
taarifa ikiwa ni pamoja na kwa Mwenyekiti au Mjumbe wa Serikali ya Kijiji,
Kiongozi wa taasisi ya dini, Diwani, Meya au Mwenyekiti wa Halmashauri au
Mbunge na kuwa viongozi hao wanatakiwa kutunza siri za taarifa walizopatiwa na
mtoa taarifa.
Katika suala
la ulinzi wa mashahidi mwezeshaji aliwaeleza Wanahabari hao ikiwa Mamlaka au
kwa maombi ya shahidi au kutokana na taarifa ilizozipata, inaona shahidi
anaweza kufukuzwa au kusimamishwa kazi, kunyanyaswa, kubaguliwa, kutishwa na
mwajiri, maisha yake au mali zake, maisha au mali za mtu wake wa karibu ziko
hatarini au kuna uwezekano wa kuwa hatarini basi mamlaka itawasilisha suala
hilo kwenye Taasisi yenye uwezo wa kumlinda shahidi. Katika kuwalinda, mamlaka
inaweza kuchukua hatua ya kumhamisha shahidi kituo cha kazi au makazi na pia
kwa madhumuni ya kuchochea hamasa ya kutoa taarifa, mtoa taarifa au shahidi
anaweza kupewa zawadi au fidia kwa utaratibu uliowekwa na Kanuni.
Katika
kuhakikisha usalama wa mtoa taarifa unazingatiwa, mwezeshaji alisema Mamlaka au
mtu yeyote anayefanya kazi za Mamlaka ambaye atatoa siri kuhusu utambulisho wa
mtoa taarifa atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atahukumiwa kifungo
kisichopungua miaka mitano au faini isiyopungua shilingi za Kitanzania milioni
15 au vyote kwa pamoja. Lakini pia Mamlaka ambayo itashindwa kuchukua
hatua kuhusu taarifa iliyotolewa na kushindwa huko kumesababisha hasara kwa
taasisi ya umma, atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atahukumiwa kifungo
kisichopungua miaka mitano au faini isiyopungua shilingi za Kitanzania milioni
15 au vyote kwa pamoja.
Lakini pia
Sheria hii pia inamwajibisha Mtoa Taarifa ambaye kwa makusudi atatoa taarifa za
uongo zinazohusu uhalifu, atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani atahukumiwa
kifungo kisichopungua mwaka mmoja au faini isiyopungua shilingi za Kitanzania
milioni 3 au vyote kwa pamoja. Pia ikiwa Mtoa Taarifa atatoa siri za mtu ambaye
taarifa za uhalifu zimetolewa dhidi yake, atakuwa ametenda kosa na akitiwa
hatiani, atahukumiwa kifungo kisichopungua mwaka mmoja au faini isiyopungua
shilingi za Kitanzania milioni 3 au vyote kwa pamoja.
Mwaka, 2016
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria hii ya kuwalinda
Watoa Taarifa za Uhalifu na Ulinzi wa Mashahidi. Wizara ya Katiba na Sheria
imepewa dhamana ya kusimamia Sheria hii ambayo imempa Waziri wa Katiba na
Sheria mamlaka ya kutengeneza Kanuni za Watoa Taarifa na Ulinzi wa Mashahidi
kwenye kifungu cha 15 cha Sura ya 446. Aidha, Wizara katika kuhakikisha Sheria
inatekelezwa kwa ufanisi na kufikia madhumuni ya sheria, kupitia mradi wa BSAAT
ilikamilisha kutunga Kanuni za Watoa Taarifa na Ulinzi wa Mashahidi (The
Whistleblower and Witness Protection Regulations) na kutangazwa kwenye gazeti
la Serikali Namba 59 la tarehe 10 Februari, 2023. Madhumuni ya kanuni hizi ni
kutoa ulinzi, motisha na kulipa fidia kwa watoa taarifa za uhalifu na
mashahidi, ili kuwaongezea imani na kuimarisha usalama wao.
Comments
Post a Comment