Elimu tuliyoipata itaondoa migogoro ya mirathi
Wanakijiji cha Kijiji cha Ngingama kata ya Linga wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi msaidizi Sehemu ya Ufuatiliaji Haki Bi. Beatrice Mpembo baada ya kikao, tarehe 26 Julai 2023.
Na
George Mwakyembe- WKS Nyasa
Wanakijiji
wa kijiji cha Ngingama Kata ya Linga Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wameshukuru
Serikali kupitia Kampeni ya Mama Samia msaada wa kisheria kwa kuwapatia elimu juu
ya mirathi ambayo imekuwa ikichangia kuleta migogoro ya ardhi katika jamii yao.
Akiongea
kwenye mkutano uliofanyika tarehe 26 Julai, 2023 katika ofisi za kata ambapo
watalaam kutoka Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na taasisi zingine za
kisheria zilitoa mada mbalimbali kama vile mirathi, ukatili wa kijinsia,
migogoro ya ardhi Mwenyekiti wa kijiji hicho ndugu Raymond Kayombo amesema
“elimu hii na iwe endelevu, binafsi sijawahi kupata elimu yeyote kuhusu
kuandika wosia pamoja na namna ya kupata mirathi, na leo ni mara yangu ya
kwanza tangu nizaliwe.”
Bw.
Kayombo akaongeza “katika kijiji chetu cha Ngingama elimu hii tuliyoipata itapunguza
migogoro ya ardhi hasa sisi tulioko huku kijijini kwasababu ardhi kubwa
tuliyonayo tumerithi kutoka kwa baba zetu ambao wengi wao walishafariki na pia
wazazi wetu hawakuandika wosia wowote.”
Naye
Oigen Charles ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ngimana amesema “fursa hii iwafikie
na wengine, mimi nilikuwa sijui masuala ya haki za binadamu lakini leo nimepata
elimu nzuri ambayo imekuwa funzo kwangu, binafsi elimu ya haki za binadamu pamoja
na elimu ya mirathi sijawahi kuisikia popote, Tumekuwa tukishuhudia vitendo vya
ukatili lakini hatukujua kama ni vya kikatili.”
Aidha,
Bi Annamaria Charles ambaye ni mzee wa miaka zaidi ya 70 amesema “suala la
wosia ni suala muhimu sana, unapofikia umri kama huu wa kwangu basi ni vyema
ukaandika ili kuacha familia isiyo na migogoro.”
Vile
vile Bi. Annamaria akaongeza “suala la mirathi hapa kijijni Ngingama limekuwa
tatizo sana, lakini kwa elimu hii wananchi wameelewa vizuri, tunaiomba Serikali
kuendelea kuwapatia elimu hii wananchi wengine hasa wa vijijini.”
Kampeni
hii itafanyika katika kata zote ishirini za Wilaya ya Nyasa na inategemea
kufikia tamati siku ya Jumatano tarehe 2 Agosti 2023.
Comments
Post a Comment