Wananchi waomba vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri zaidi ya miaka mitano vitolewe kwenye Ofisi za Kata

Bw. Mwinyijuma Maneno Moshi Afisa Msajili Msaidizi RITA na mtaalam kwenye timu ya kutoa msaada wa sheria ya Mama Samia akitoa elimu ya Usajili wa Vizazi na Vifo kwenye mkutano uliofanyika ofisi za Kata ya Chiwana wilaya ya Tunduru, 26/07/2023.

 

Wakili Gloria Baltazari kutoka Chama cha Mawakili Tanganyika na mtaalam kwenye timu ya kutoa msaada wa sheria ya Mama Samia akitoa elimu ya sheria kwenye mkutano uliofanyika ofisi za Kata ya Chiwana wilaya ya Tunduru, 26/07/2023.

Bw. Nelson William Afisa Ustawi wa Jamii na mtaalam kwenye timu ya kutoa msaada wa sheria ya Mama Samia akitoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwenye mkutano uliofanyika ofisi za Kata ya Chiwana wilaya ya Tunduru, 26/07/2023

                                           xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Na William Mabusi – WKS Tunduru

 

Wananchi wa vijiji vya Chiwana, Umoja na Mkandu wilayani Tunduru wameiomba Serikali kuweka utaratibu ili vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri zaidi ya miaka mitano navyo vitolewe kwenye Ofisi za Kata kama ilivyo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ili kuwapunguzia gharama na muda wa kufuatilia vyeti hivyo kwenye ofisi za Wilaya ambazo kwa baadhi ya Kata ofisi hizo ziko mbali.

Ombi hilo limetolewa kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara iliyoitishwa na timu inayotekeleza kampeni ya msaada wa sheria ya Mama Samia Wilayani humo, tarehe 26 Julai, 2023.

“Tunaipongeza Serikali kwa kusimamia utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano kwenye ofisi za Kata. Tunaiomba Serikali kuweka utaratibu ili watoto wenye umri zaidi ya miaka mitano nao waweze kupata vyeti vyao kwenye ofisi zetu za Kata.” Alisema mzee Mapepe Said kutoka Kijiji cha Chiwana.

 

Akitoa elimu ya usajili wa vizazi na vifo kwenye mikutano hiyo Bw. Mwinyijuma Maneno Moshi Afisa Msajili Msaidizi kutoka RITA ambaye yuko kwenye timu ya wataalam wanaotekeleza Kampeni hiyo amesema watoto walio na umri chini ya miaka mitano husajiliwa bure bila malipo na kupewa vyeti vya kuzaliwa ndani ya siku tisini tokea mama alipojifungua.

Kampeni hiyo ilizinduliwa na Mhe. Dkt. Philip Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Julai, 2023 mjini Songea na mara baada ya uzinduzi wataalam waligawanyika kutekeleza kampeni hiyo kwenye Halmashauri zote nane katika Mkoa wa Ruvuma.

Timu ya wataalam wanaotekeleza Kampeni hiyo Wilayani Tunduru imeshafikia Kata nane kati ya ishirini zinazotakiwa kutekelezwa katika kipindi cha siku kumi tangu kuzinduliwa kwa Kampeni hiyo mkoani Ruvuma. Kata ambazo zimefikiwa hadi sasa ni Muungano, Nanjoka, Nakapanya, Nandembo, Lukumbule, Mchoteka, Marumba na Chiwana.

 


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA