MoCLA YAOMBWA KUONGEZA USHIRIKIANO NA WAZEE WA KIMILA NA VIONGOZI WA DINI


 Mzee Isack Olekisongo Meijo ambaye ni Chifu Mkuu wa Wamasai Tanzania mwenye umri wa Miaka Sabini akiongelea umuhimu wa Wizara kuwa karibu na Viongozi wa Kimila


Mwanasheria kutoka shirika la watoa msaada wa kisheria la CSP bwana Eliakim Paulo akitoa elimu ya sheria kwa viongozi wa kimila na wa dini waliohudhuria warsha hiyo.


 Mmoja wa wazee wa kimila waliohudhuria warsha hiyo akichangia maada zilizokuwa zinajadiliwa.


Sehemu ya washiriki wa warsha hii ya siku mbili iliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi hao.

                                                XXXXXXXXXXXXXXXXXX

Na Lusajo Mwakabuku – WKS Babati

Wazee wa Kimila wa viongozi wa dini wametoa wito kwa uongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria kuongeza ukaribu na viongozi hao kwani wao ndio wapo karibu na jamii katika masuala la malezi kwa watoto na vijana kimaadili ili kuweka mustakabali wa Taifa na watu wake kwenye mikono salama.

Wazee na viongozi hao wameyasema hayo leo 07/08/2023 katika warsha ya siku mbili iliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi hao kwenye masuala ya kisheria katika majukumu yao ya kila siku hususan kwenye kufanya usuluhishi wa migogoro mbalimbali na kudhibiti vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.

Wakiongea wakati wa majadiliano baada ya kutolewa mada mbalimbali kutoka kwa wataalam wa sheria kutoka wizarani na taasisi binafsi, wazee hao walibainisha kuwa wao wapo karibu na wananchi na kila siku wanakutana na mambo mengi ambayo mengine yanapaswa kupatiwa ufumbuzi katika ngazi ya wizara na hivyo kukiwa na ushirikiano wa karibu kutarihisisha utatuzi wa migogoro na kuipunguzia mahakama mzigo wa kesi.

“Sisi tunakutana na wananchi wetu katika maeneo yetu angalau kila wiki hasa viongozi wetu wa dini ambao kila Jumapili kwa wakristu na Ijumaa tunapata nafasi ya kusikiliza na kutatua kero nyingi na sisi tunakuwa na taarifa nyingi ambazo wizara ikizipata inaweza kuwa katika sehemu nzuri zaidi ya kuboresha usimamizi wa haki” Alisema Chifu Mkuu wa Wamasai Tanzania Isack Olekisongo Meijo

Aidha Chief Meijo aliongeza kuwa vijana wakifundishwa vizuri mila, desturi na maelezo ya kitaalam kutoka kwa wataalam huku wakikukbushwa kushika mafundisho ya dini na wakawa na hofu ya Mwenyezi Mungu maovu mengi ikiwemo ndoa za jinsia moja, ulawiti na unyanyasaji wa kijinsia vitapungua kwa kiwango kikubwa hapa nchini.

Akiongelea madhuminu ya kuitisha warsha hii, Wakili wa serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria George Mollel alisema serikali inatambua umuhimu wa madhehebu ya Dini na viongozi wa dini kuwa ni sehemu muhimu katika kuimarisha amani katika jamii na ndio maana serikali inaendelea kushirikiana nao katika kujenga maadili mema kuanzia ngazi ya familia na jamii kwa ujumla

Mwanasheria kutoka shirika la watoa msaada wa kisheria linalojulikana kwa jina la CSP bwana Eliakim Paulo akitoa elimu ya jinsi sheria za nchi zinavyotekelezwa kwa viongozi hao alisema elimu inayotolewa kwa wazee hao itatumika kuwasaidia katika kuleta mabadiliko kwenye jamii zao ikiwemo kupambana na ukatili wa kijinsia, kuchochea usawa wa kijinsia, kusomesha watoto wa kike na wanawake kushiriki kwenye shughuli za kimaendeleo.

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA