NDUMBARO AHIMIZA USHIRIKIANO BAINA YA TAASISI ZA SERIKALI NA WADAU KATIKA UPATIKAJI HAKI.


 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro  akiongea na wadau wa haki walihudhuria kongamano hilo jijini Arusha tarehe 17  - 18 Agosti 2023.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo akiwahutubia wadau wa haki walihudhuria kongamano hilo jijini Arusha tarehe 17  - 18 Agosti 2023.


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro  akibadilishana mawazo na Makamu Mwenyekiti wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Bi. Lulu Ng’wanakilala wakiwa katika mapumziko mafupi ya kongamano hilo.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro  akiwa katika picha ya pamoja na wadau na menejimenti ya Wizara ya katiba na Sheria.

Na. Lusajo Mwakabuku WKS - Arusha 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amezitaka taasisi za Serikali hususani zinazoshughulika na masuala ya upatikanaji wa haki, Mahakama pamoja na Bunge kufanya kazi kwa pamoja na wadau wote wa huduma za msaada wa kisheria na upatikanaji wa haki nchini kwa manufaa ya watanzania wote.

Ndumbaro ameyasema hayo wakati akizindua Kongamano la Huduma za Msaada wa Kisheria linaloendelea katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha kwa siku mbili tarehe 17 – 18 Agosti mwaka huu. 

“Katika kufikia upatikanaji wa haki yenye usawa, juhudi za makusudi zinahitajika katika kuimarisha ushirikiano kati yenu na mamlaka nyingine za Serikali, Mahakama na Bunge kwa nia ya kuboresha utendaji kazi wa taasisi za utoaji haki nchini. Tutumie fursa zilizopo kujenga mahusiano mazuri yatakayochochea ubora wa huduma za msaada wa kisheria kwa jamii” Alisema Dkt, Ndumbaro.

Akiongelea umuhimu wa kongamano hilo, Mhe. Ndumbaro aliwataka wajumbe wa kongamano hilo kuzingatia weledi, uadilifu, uzalendo kwa manufaa na umuhimu wa nafasi zetu familia, jamii na Taifa kwa ujumla. Pia Ndumbaro alisisitiza wadau wa haki kuwa na taarifa sahihi kabla kuchukua hatua au kusema huku akisisitiza matumizi ya tafiti na takwimu kwenye miradi na program mbalimbali zinazoweza kutoa majawabu ya changamtoto mbalimbali katika jamii.

Akikazia suala la kuimarisha ushirikiano baina ya wadau, Ndumbaro aliwataka wadau hawa kuacha kujiangalia wenyewe, huku akitumia methali isemayo ‘kidole kimoja hakivunji chawa’ napia akatumia misemo ya kiingereza yanayosema  ‘if you want go fast go alone, if you want to reach far go together’. 

Aidha, Ndumbaro aliwahimiza kufuatilia, kusimamia na kufanyia kazi mapendekezo mbalimbali yatakayotokana na Kongamano hili katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo ili kukidhi malengo ya kuanzishwa kwa Mashirika yao na matarajio ya jamii ya Watanzania wanaowahudumia.

Akitoa salamu za awali kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Bi Mary Makondo alisema Kongamano hili linalohusika moja kwa moja na kampeni kubwa ya miaka mitatu iliyopewa jina la Mama Samia Legal Aid Campaign limelenga kuhakikisha kuwa matokeo yanayotokana na kampeni hii yanakuwa na tija kwa wananchi wote bila kujali matabaka ya kiuchimi, kijinsia na kuboresha maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

“Matokeo ya muda mrefu wa Kampeni hii ni kuchangia katika kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususani wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi. Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kisiasa hapa nchini. Ninatambua kuwa baadhi ya washiriki wa Kongamano hili ni washiriki katika Kampeni ya msaada wa Kisheria ya (Mama Samia Legal Aid Campaign) na iwapo mmeweza kubaini changamoto mbalimbali katika Kampeni hiyo tunaomba kupitia Kongamano hili mzibainishe ili Wizara iweze kuzifanyia kazi” Alisema Bi. Makondo.

Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau inatekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya (Mama Samia Legal Aid Campaign) ambayo ilianza kutekelezwa Jijini Dodoma mnamo tarehe 27 Aprili, 2023 baada ya kuzinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) tarehe 27 Mei, 2023 Jijini Dodoma. Kampeni hii inafanyika kwa miaka mitatu kuanzia mwezi Machi, 2023 hadi mwezi Februari, 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.


 

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA