DKT. CHANA AITAKA TUME KUWA NA MKAKATI WA KUZUIA UVUNJIFU WA HAKI ZA BINADAMU
Waziri wa Katiba n Sheria Mhe. Balozi Dkt Pindi Chana akihutubia kwenye kikao na Wafanyakazi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tarehe 07 Septemba 2023 Jijini Dodoma.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na
William Mabusi, Emmanuel Msenga na Faraja Mhise – WKS Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
ametoa wito kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini kuwa na mkakati
wa kuzuia mambo yanayosababisha uvunjifu wa haki za binadamu ili hali ya amani
iendelee kutawala nchini.
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo
alipotembelea ofisi za Tume hiyo maeneo ya Kilimani na kuhutubia wafanyakazi wa
ofisi hiyo tarehe 07 Septemba, 2023 Jijini Dodoma.
“Pamoja na kuandika na kutoa taarifa za uvunjifu wa haki
za binadamu nchini lakini pia
tuwe na mkakati wa kuzuia mambo hayo yasitokee na eneo sahihi la kutekeleza
hili ni Tume yetu inayoshughulikia masuala ya haki za binadamu
na utawala bora.” Alisema Dkt. Chana.
Balozi Dkt. Chana ameipongeza Tume kwa kuendelea
kufanya tafiti za uvunjifu wa haki za binadamu nchini na kuandaa taarifa ambazo
huwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana ili aziwasilishe Bungeni zisomwe. Waziri
Chana akatumia fursa hiyo kulipongeza Bunge kwa kukubali taarifa za Tume hiyo
kusomwa Bungeni, "hiyo ni hatua kubwa na nzuri kwa Bunge kukubali kupokea
taarifa za Tume ambazo zimeanza tena kusomwa Bungeni mwezi Machi mwaka huu.”
Aidha, Mhesimiwa Waziri ameahidi kuhakikisha Tume
inakuwa na ofisi za uhakika kwani Tume ni chombo cha Kikatiba, “Lazima tuwe na
Ofisi za uhakika maana hii ni tume ya kikatiba iko ndani ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Tuwe na ofisi za Uhakika Dodoma na kwenye mikoa
mingine ambako tayari Tume ina ofisi na
ofisi za Kanda zinazotarajiwa kujengwa.”
Mhe. Chana amezungumzia ustawi wa watumishi na kutoa
ahadi ya kuboresha maslahi yao “ukitaka kupata maziwa mengi kwenye ng’ombe
lazima umlishe vizuri, vivyo hivyo tutatoa kipaumbele kwenye maslahi na haki ya
watumishi ili waweze kufanya kazi vizuri zaidi,” alisema
Mhe. Chana.
Awali akitoa taarifa ya Tume, Mwenyekiti wa Tume Mhe.
Methew Mwaimu (Jaji Mstaafu) amesema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
ni idara ya Serikali inayojitegemea na imeundwa kwa mujibu wa ibara namba 129
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria ya Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora sura 391 ambayo imeweka utaratibu jinsi Tume
inavyotekeleza majukumu yake ya msingi kuwa ni kuhamasisha kwa kutoa elimu kwa
umma kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.
Majukumu mengine ya Tume ni pamoja na kulinda haki za binadamu,
hupokea na kufanya uchunguzi wa malalamiko yanayohusu uvunjaji wa haki za
binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa mtu mmoja mmoja au
taasisi, Tume hufanya utafiti kuhusu masuala mbalimbali ambayo ni changamoto
katika utoaji haki na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na misingi
ya utawala bora, kutembelea Magereza na sehemu zingine za vizuizi kwa lengo la
kutathmini na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha hali ya uzingatiwaji
wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa wafungwa na waliozuiliwa
katika sehemui hizo.
Comments
Post a Comment