GEKUL ASHIRIKI “UTU KWANZA RUN” DAR ES SALAAM
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Pauline Gekul akizindua mradi wa Dawati la Msaada wa Kisheria (Legal Aid Desk
Project), tarehe 10 Septemba, 2023 Jijini Dar es Salaa
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Pauline Gekul akishiriki mbio kwenye hafla ya Utu Kwanza Run ambapo alikimbia
kilomita tano, tarehe 10 Septemba, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul akiwasilisha hotuba yake kwenye hafla ya Utu kwanza Run kwenye Viwanja vya Leaders Club tarehe 10 septemba 2023 Jijini Dar es slaam .
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Naibu Waziri
wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul akimwakilisha Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, ameungana na Wakimbiaji, Watembeaji na
Waendesha Baiskeli walioshiriki “Utu Kwanza Run” tarehe 10 Septemba, 2023
Jijini Dar es Salaam.
Mbio hizo
zilizoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali (NGO) la Utu Kwanza, chini ya
Uenyekiti wa Wakili Shehzada Amir Walli zimelenga kujitoa kwa hali na mali
katika kutekeleza jukumu la kuboresha maisha ya Mahabusu na Wafungwa, familia
za hao Mahabusu na Wafungwa, pamoja na kuangalia namna bora ya kuboresha maisha
ya Maofisa wa Magereza wanaoishi na kuwajibika moja kwa moja na usimamizi wa
Mahabusu na Wafungwa nchini.
Akiongea
katika hafla hiyo, Gekul amesema malengo ya Utu Kwanza yanakwenda sambamba na
maono ya Serikali ya Awamu ya Sita kwani Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kujali utu, aliunda tume maalum ya kupitia na kutoa mapendekezo ya
kurekebisha mfumo wa haki jinai nchini ambayo imefanya kazi kubwa kwa kuzunguka
nchi nzima ikikusanya mawazo kwa Wananchi na Wadau wote wa Sheria ili kuboresha
Mfumo mzima wa Haki Jinai Nchini.
“Ndio maana,
sisi kama Wizara ya Katiba na Sheria, hatukusita kupokea wito na kushiriki
kwenye Hafla hii ya Utu Kwanza baada ya kuridhishwa na Malengo na kazi nzuri
inayofanywa na Shirika hili la Utu Kwanza sambamba na jitihada za Serikali ya
Awamu ya Sita katika kuboresha maisha ya Watanzania wote bila kujali rangi,
itikadi, jinsia wala asili kwenye Sekta ya Upatikanaji wa Haki, na hasa Haki
Jinai – ambako ndiko linapopatikana kundi la mahabusu na wafungwa.” Alisema
Gekul.
Aidha Mhe.
Gekul alitumia nafasi hiyo kuyataka mashirika mengine yanayojihusisha na utoaji
wa msaada wa kisheria kutumia rasilimali zao vizuri ili kuwafikia walengwa na
kushirikiana na Serikali katika kuboresha maisha ya watu wote huku akitaja utu
kuendelea kuwa kipaumbele kwenye HAKI JINAI na na kuhakikisha wote tunatimiza
wajibu wetu katika kuwatumikia Watanzania na kudumisha amani na mshikamano
ambazo ni tunu muhimu kwa maendeleo na ustawi wa Taifa letu.
Pia Gekul
amewapongeza Utu Kwanza kwa kuanzisha Mradi wa Dawati la Msaada wa Sheria,
(LEGAL AID DESK) akisema kuwa dawati hilo licha ya kupokea changamoto
mbalimbali za kisheria pia litatumika kama chanzo kingine cha fedha kwa ajili
ya kuwahudumia wananchi wengine.
“Mradi huu
ukisimamiwa vizuri, utakuwa ni jawabu zuri kwa Umma na Watanzania walio wengi
wanaohitaji msaada wa dharura hasa pale wanapopatwa na matatizo ya kijinai.
Watanzania na Jamii, watumie fursa hizi vizuri ili watu wasio na uwezo wa
kupata msaada wa kisheria kwa gharama za kulipia, wapate msaada unaostahili,”
aliongezea Mhe. Gekul.
Comments
Post a Comment