MSLAC YAREJESHA VIWANJA VIWILI ALIVYOPORWA MWANANCHI
Bi. Mboje Masanja Ndahile Mkazi wa eneo la Imalilo Kata ya Bunamhla , Halmashauri ya Mji wa Bariadi akifurai baada ya kurudishiwa shamba lake kupitia Mama Samia Legal Aid Campain mkoani Simiyu.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na
William Mabusi – WKS Bariadi
Mgogoro uliodumu kwa miaka
miwili kati ya Bi. Mboje Masanja Ndahile Mkazi wa eneo la Imalilo Kata ya
Bunamhla na Halmashauri ya Mji wa Bariadi ambao haukumpa matumaini ya kupata
viwanja vyake viwili umetatuliwa na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia
(Mama Samia Legal Aid Campaign - MSLAC) kwa siku tatu na mama huyo kurejeshewa
viwanja vyake.
Jitihada za kupata viwanja
hivyo zilikuwa zimegonga mwamba kwani kila alipokuwa anafuatilia aliambiwa
Serikali imechukua viwanja hivyo ili kupanga mji na hakukuwa na namna nyingine
ya kuvipata. “niliposikia kuna kongamano la sheria na watu wanasaidiwa nilikuja
na kuonana na wataalam wa sheria akiwepo kiongozi wenu na akaagiza nipate
viwanja vyangu na kweli nimevipata hizi hapa barua za kurejeshewa viwanja hivyo.”
Alisema huku akionesha nakala hizo alipokuwa amerudi kushukuru timu ya MSLAC
iliyokita kambi kwenye viwanja vya Stendi ya zamani Mjini Bariadi tarehe 23
Septemba, 2023.
Bi. Mboje alifika viwanja
hivyo na kuonana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary
Makondo tarehe 20 Septemba, 2023 aliyekuwa viwanjani hapo kujionea mwenyewe
utekelezaji wa Kampeni hiyo inayoendelea kutekelezwa kwenye Halmashauri zote
sita Mkoani Simiyu. Baada ya kuridhishwa na maelezo yake Bi. Makondo aliagiza
watumishi wa Kitengo cha Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuhakikisha
mama huyo anapatiwa haki yake.
Comments
Post a Comment