WAZIRI CHANA AKEMEA MIMBA ZA UTOTONI
Meza Kuu ikiwa kwenye picha ya
pamoja na Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria bada ya uzinduzi wa Mama
Samia Legal Aid Campaign mkoani Simiyu tarehe 18 Septemba, 2023 Mjini Bariadi
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
akihutubia wakati anazindua utekelezwaji wa Mama Samia Legal Aid Campaign
mkoani Simiyu tarehe 18 Septemba, 2023 Mjini Bariadi.
Na
William Mabusi & Lusajo Mwakabuku – WKS Simiyu
Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (MB) amekemea mimba za utotoni
akiwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanahudhuria shuleni kwa faida
yao ya baadaye na kujenga taifa imara, lenye kizazi bora na wataalam wengi
zaidi.
Mhe. Waziri
Chana ameyasema hayo wakati akihutubia mamia ya wananchi wa mji wa Bariadi
waliohudhuria uzinduzi wa utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Mama Samia Legal
Aid Campaign tarehe 18 Septemba, 2023. Kampeni hiyo itafanyika mkoani humo kwa
siku kumi kwa kutoa elimu ya sheria na utatuzi wa migogoro mbalimbali bure.
Mkutano huo
pia umehudhuriwa na Wakuu wote wa Wilaya za Mkoa wa Simiyu, Wenyeviti wa
Halmashauri, Bodi ya Taifa ya Ushauri kwa Watoa Huduma ya Msaada wa Kisheria.
Viongozi mbalimbali akiwemo Mhe. Pauline Gekul Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria, Mhe. Mashimba Ndaki Mbunge wa Maswa Magharibi ambaye pia ni mjumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Selemani Zedi
Mbunge wa Bukene ambaye pia alimwakilisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria na ndugu Abdulhaman Mshamu aliyemwakilisha
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria.
“Kwa tafsiri
mimba za utotoni ni ukatili wa kijinsia. Huwezi ukasema mtoto chini ya
miaka 18 alitoa ridhaa huo ni ukatili. Ndiyo maana watoto chini ya umri wa
miaka kumi na nane hawaruhusiwi kupiga kura wala kupewa kibali cha kuendesha
boda boda.” Alisema mheshimiwa Waziri na kuwataka watanzania wote kusema “stop”
kwa ukatili wa kijinsia na kila mmoja kwa nafasi yake na uwezo wake awe mlinzi
wa mwenzake.
Amewataka
wazazi na walezi kuhakikisha watoto wa umri wa kwenda shule wanaenda shule ili
wapate elimu ambayo itakuja kuwasaidia baadaye. “Wakati wa kutumia watoto
kwenda kuchunga mifugo umekwisha, watoto lazima waende shule wapate elimu ili
nchi iwe na wataalam wengi zaidi, aidha, elimu watakayopata wataitumia kuongeza
thamani ya mifugo tulinayo mfano ukichinja ng’ombe watajua ngozi itumie vipi au
pembe zitumike vipi.
Mhe. Chana
ameyashukuru Mashirika na Asasi mbalimbali ambazo zimeendelea kuunga mkono na
kuwa mstari wa mbele kulinda haki na ulinzi wa mtoto, kupinga ukatili dhidi ya
wanawake na watoto na kutoa elimu ya kisheria na haki za binadamu na kuyataka
kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha uvunjifu wa haki za
wanawake, wanaume na watoto na makundi maalumu unatokomezwa nchini.
Amewapongeza
na kuwasihi viongozi wa dini kuendelea kukemea vitendo viovu, kuendelea
kuisaidia na kushirikiana na Serikali kwa kuwafundisha waumini na wafuasi wa
dini zao kufuata sheria za nchi, kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia na
aina nyingine za uhalifu katika jamii katika jitihada za kujenga jamii yenye
maadili mema na yenye hofu ya Mungu ambao chanzo chake ni kuheshimu haki za
binadamu. Aidha, Mhe. Waziri amevipongeza na kuvitaka Vyombo vya Habari
kuendelea kutoa taarifa za uvunjifu wa amani na ukatli wa kijinsia, kuendelea
kutoa uelewa kwenye jamii juu ya masuala ya haki za binadamu na sheria ili
kuepusha watu kufanya mambo yao kienyeji pasipo kufuata sheria za nchi.
Kwa upande
wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amesema amefurahishwa
na kauli ya Mhe. Mashimba Ndaki Mbunge wa Maswa Magharibi aliposema kuwa Simiyu
hakuna migogoro ya ndoa na kwamba hilo ni jambo jema katika ustawi wa jamii
yetu ila akatoa rai kwa wananchi kuzifahamu haki zao katika ndoa.
“Nimefurahiswa
sana na maelezo yake mbunge mwenzangu Mhe. Mashimba Ndaki Mbunge wa Maswa
Magharibi, aliposimama hapa amesema Simiyu hakuna migogoro ya ndoa, lakini
naomba niwaambie ni muhimu sana kufahamu haki zenu kuwa mke wa kwanza haki zake
ni zipi, mke wa pili na kadhalika, nasema haya kwani matatizo ya mirathi mengi
yanachangiwa pia na watu kutokujua haki zao” alisema Mhe. Gekul.
Awali
akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Ismail Nawanda
amepongeza kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Simiyu ambapo
hivi karibuni amewapa fedha za mradi wa maji kutoka ziwa Victoria ambao
unategemewa kukamilika baada ya miaka mitatu toka sasa.
Dkt. Nawanda
amesema mkoa wake umejipanga kuona malengo na matarajio ya Mhe. Rais kuhusu
Kampeni ya Mama Samia yanafikiwa na kuahidi Simiyu itakwenda kuvunja rekodi kwa
wananchi wengi kuhudhuria kwenye mikutano kupata elimu ya sheria na pia mkoa
kuendelea kutoa huduma ya msaada wa kisheria baada ya siku kumi za
Kampeni hiyo kukamilika.
Naye Mhe.
Mashimba Ndaki Mbunge wa Maswa Magharibi akiwakilisha Wabunge wa Mkoa wa Simiyu
amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na maono ya kupeleka
haki na usawa kwa wananchi wa chini. “Pamoja na huduma za jamii anazotoa kwa
watanzania bado akaona bila haki wananchi hawatakuwa na amani, hawatafikia
maendeleo ambayo anataka wayapate na kukubali Kampeni hii kufanyika nchi
nzima.” Alisema Mhe. Ndaki.
Utekelezaji
wa Kampeni hiyo ni agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la
kuwafikia wananchi wa chini kabisa wasio na uwezo, kusikiliza hoja zao, kero
zao na kisha kuwasaidia kwa kuwashauri, kuwapa elimu na kutatua kero hizo.
Katika kutekeleza Kampeni hii mkoani Simiyu, Wilaya zote tano na Halmashauri
sita zitafikiwa ambapo wananchi wa Kata zisizopungua Hamsini watahudumiwa kwa
kupewa elimu ya sheria na utatuzi wa migogoro mbalimbali.
Kampeni hii
inafanyika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar. Tangu kuanza kwa kampeni hii
huu ni mkoa wa tano kwa upande wa Tanzania Bara tangu ilipozinduliwa na
kuanza kutekelezwa Mkoa wa Dodoma na baadaye Manyara, Shinyanga, Ruvuma ambapo
hadi sasa wananchi laki mbili na themanini (280,000) wamehudumiwa, laki moja na
nusu wanawake na wanaume laki moja na elfu thelathini.
Comments
Post a Comment