WAZIRI KATIBA NA SHERIA AIPONGEZA MAHAKAMA KWA KUIHESHIMISHA TANZANIA KIMATAIFA
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na
Viongozi wengine kwenye picha ya pamoja na wageni wake – Waziri wa Katiba na
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria walipomtembelea na kufanya mazungumzo ofisini
kwake jijini Dar es Salaam, 15/09/2023.
Na. Faustine Kapama-Mahakama na Sade
Soka-UDSM
Waziri wa
Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana tarehe 15 Septemba, 2023 amemtembelea
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake jijini Dar
es Salaam na kufanya naye mazungumzo mafupi ambapo ameipongeza Mahakama ya
Tanzania kwa kuiheshimisha Tanzania kimataifa.
Mhe. Balozi
Chana, ambaye aliongozana na Naibu Waziri, Mhe. Pauline Gekul na Mkurugenzi wa
Huduma za Sheria kwa Umma kutoka Wizara hiyo, Bw. Abdulrahman Mshamu, amesema
Tanzania ni miongoni mwa Nchi ambayo masuala ya utawala wa Sheria yanazingatiwa.
“Tunapata
fursa wakati mwingine kwenda Nchi mbalimbali, ukienda huko duniani ndipo
utakapojua kwamba Tanzania tupo vizuri. Niliwahi kwenda (sehemu) nikaambiwa
hapa hakuna Bunge, Mahakama haieleweki, kwa kweli sisi tupo mbali. Mhimili wa
Mahakama unatuheshimisha kama Taifa, tunakupongeza sana,” Waziri Chana
alimwambia Jaji Mkuu.
Ameeleza
dhumuni la kumtembelea ni kujitambulisha na kujifunza mambo mbalimbali
yanayofanyika katika Wizara yake, kama alivyofanya kwenye taasisi zingine,
ikiwemo Shule ya Sheria kwa Vitendo na kuahidi kushirikiana na Mahakama
kushughulikia mambo kadhaa ya kiutendaji yanayoikabili Shule hiyo.
“Tunawaomba
sana msiache kutushauri kuhusu suala hili la Shule ya Sheria kwa Vitendo, ninyi
mmebobea kwenye vyuo hivi, mnaweza kushauri tuboreshe wapi, haiwezekani kwa
nini watu walalamike kuwa hawafaulu kwenye masomo yao. Milango yetu ipo wazi,
mkitaka maboresho ya bajeti, sheria na kanuni, haya ni majukumu yetu, sisi
tutakuwa tayari muda wowote,” amesema.
Naye Naibu
Waziri amemshukuru Jaji Mkuu kwa kuimarisha utendaji katika Mahakama ya
Tanzania kwani picha iliyopo huko nje, hasa katika Magereza, ni nzuri kwani
wafungwa na mahabusu wanaridhishwa na kasi ya usikilizaji wa mashauri yao.
“Picha
iliyoko huko ni nzuri kwa kweli, tumekuwa tukitembelea Magereza tunakutana na
mahabusu na wafungwa, wanawapongeza sana na wamefurahi namna wanavyo angaliwa
vizuri na Mahakama, nakala zao za hukumu wanazipata kwa wakati, kesi
zinasikilizwa, hivyo wanaishukuru Mahakama kwa kazi hii nzuri,” amesema.
Kadharika,
amemshukuru Mhe. Prof. Juma kwa kuwawezesha kama Viongozi wa Wizara ya Katiba
na Sheria kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mahakama, hatua
inayomsaidia kujibu kwa ufasaha maswali anayokutana nayo Bungeni.
“Naupongeza
Uongozi wa Mahakama kwa kushirikiana nami na kuwa tayari kunisaidia katika
hatua mbalimbali, ikiwemo kujibu maswali ninayoyapata Bungeni, hasa suala hili
la miradi inayoendelea kutekelezwa, ikiwemo ujenzi wa Mahakama za Mwanzo 60,”
amesema.
Akizungumza
na wageni wake, Jaji Mkuu alimpongeza Waziri Chana kwa kuaminiwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na
Mhimili wa Mahakama.
Amemkaribisha
kuitembelea Mahakama mara kwa mara ili kujifunza shughuli mbalimbali
zinazofanywa na Mhimili huo.
“Kuna maeneo
ambayo yanasukuma maboresho ya Mahakama. Kitengo cha Maboresho ni injini, haya
maboresho yanayoendelea kuna watu ambao wapo masaa 24 wakiangalia kitu gani
kipo wapo, majengo yakoje, TEHAMA ipo vipi, tuna Kituo Jumuishi cha Masuala ya
Familia, ni Dunia nyingine kabisa. Hivyo, haya ni maeneo ambayo ni muhimu sana
ukiyaelewa,” Mhe. Prof. Juma amemweleza Waziri Chana.
Jaji Mkuu
amemshukuru Waziri kwa kuendelea kuiongelea Mahakama katika maeneo mbalimbali,
ikiwemo Bungeni kwa kuzingatia mambo mengi yanayofanyika hayafahamiki kwa umma
kwa kiwango cha kuridhisha. “Ukisoma kwenye magazeti kuhusu Mahakama au Wizara
utashangaa kama hao wanaoandika wanaishi Tanzania. Nadhani tunajukumu la
kuuhabarisha umma,” amesema.
Kuhusu Shule
ya Sheria kwa Vitendo, Mhe. Prof. Juma amekubaliana na Waziri kuwa ni eneo
ambalo wanahitaji kulifanyia kazi kwa kushirikisha Wizara na Mahakama kwa
pamoja ili kutafuta namna ya kutatua changamoto zinazoibuliwa, hasa katika kuimarisha
elimu kwa vitendo kwa wanafunzi.
Kwa upande
wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani
amesema Mahakama imekuwa ikishirikiana na Shule ya Sheria kwa Vitendo katika
kufanya maboresho na kuanzia Januari mwakani wanatarajia kutakuwa na mitaala
mipya, hatua ambayo itasaidia kubadilisha hali ya Shule hiyo.
“Toka mwanzo
ilionekana elimu iliyokuwa inatolewa ilikuwa nadhalia zaidi, ile practical aspect ambayo
inatarajiwa wanafunzi wanapokuwa katika hatua za mwisho kabisa za kuhitimu
taaluma yao waipate ilikuwa changamoto. Kwa hiyo, Mahakama imeshiriki kwenye
maboresho makubwa,” amebainisha.
Jaji
Kiongozi ameshukuru mtazamo wa Wizara kuhusu Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto kwani ni rahisi zaidi baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu kama
kitakuwa moja kwa moja chini ya Mahakama, hatua ambayo itaimarisha zaidi
utendaji wake.
Akizunguza
katika tukio hilo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel alimfahamisha Waziri maeneo manne ambayo wanaweza kuyatembelea, Kituo
Jumuishi cha Masuala ya Familia, Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya
Tanzania, Kituo cha Huduma kwa Mteja Kinondoni, Tume ya Utumishi wa Mahakama na
Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara.
Comments
Post a Comment