Pelekeni kwa Wananchi Elimu ya Sheria Mliyopata: Dkt. Kazungu
Bw. Burton Mwasomola Mkurugenzi Msaidizi wa
Katiba kutoka Wizara ya Katiba na Sheria akihutubia kwa niaba ya Naibu Katibu
Mkuu Dkt. Khatibu Kazungu wakati wa kufunga mafunzo ya Sheria ya Ulinzi wa Watoa
Taarifa na Mashahidi ya mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2023, tarehe 13
Oktoba, 2023 Morogoro.
Na William Mabusi – WKS Morogoro
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na
Sheria Dkt. Khatibu Kazungu ametoa rai kwa washiriki wa mafunzo ya Sheria ya Ulinzi
wa Watoa Taarifa na Mashahidi ya mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2023 kupeleka
elimu waliyoipata kwa wananchi ili watambue jitihada zinazofanywa na Serikali
za kuendelea kupambana na uhalifu nchini.
Dkt. Kazungu ametoa rai kwenye hotuba yake
iliyosomwa kwa niaba yake na Bw. Burton Mwasomola Mkurugenzi Msaidizi wa Katiba
wakati wa kufunga mafunzo ya Sheria ya Ulinzi wa Watoa Taarifa na Mashahidi ya
mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2023 kwa Maafisa Waandamizi Wachunguzi
kutoka Taasisi Chunguzi na Waendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,
tarehe 13 Oktoba, 2023 Mkoani Morogoro.
“Rai yangu mkaendelee kutoa elimu kwa umma wa
watanzania na watumishi wenzenu kuhusiana na malengo ya Sheria hii na Kanuni
zake ili wafahamu umuhimu wa kuwafichua wahalifu wa makosa mbalimbali ili
hatimaye kutokomeza mtandao wa uhalifu nchini,” alisema.
Dkt. Kazungu aliongeza kuwa, “katika
kutekeleza majukumu yenu mna watu ambao huwatumia kuwapa taarifa za uhalifu,
kupitia mafunzo haya kawaambieni kwamba Serikali imeweka utaratibu wa ulinzi
kwao pale ambapo itaonekana maisha yao yako hatarini kutokana na taarifa za
uhalifu watakazotoa.”
Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wengine, aliyekuwa Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Wakili wa Serikali Bi. Florida Wenceslaus amesema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa wa Sheria ya Ulinzi wa Watoa Taarifa na Mashahidi ya mwaka, 2015 na Kanuni zake za mwaka 2023 na hivyo kwenda kurahisisha utendaji kazi wao kwani utekelezaji wa Sheria hiyo utawapa hamasa wananchi kutoa taarifa za uhalifu.
Comments
Post a Comment