RAIS DKT. SAMIA ATUNUKIWA TUZO YA HESHIMA NA TUME YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Balozi Pindi
Chana(Mb)akipokea Tunzo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Viongozi wa Tume
ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Oktoba 21,2023 Arusha.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na Lusajo Mwakabuku
& Rosemary Mlale - Arusha
Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imemtunukia Tuzo
ya Heshima Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kutambua mchango wake katika kutetea, kulinda na kuimarisha haki za
binadamu katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.
Balozi Dkt. Pindi Chana kwa niaba ya Mhe. Rais Samia wakati wa kilele cha
maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu Afrika na maadhimisho ya miaka 20 ya
Itifaki ya Maputo kuhusu Haki za Wanawake yaliyofanyika jijini ARusha tarehe 21
Oktoba 2023.
Akieleza sababu za kumtunuku Mhe. Rais Dkt Samia tuzo hiyo,
Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Janet Ratatouille Sallah-njie amesema Mhe.
Rais Dkt. Samia amekuwa kiongozi wa mfano barani Afrika katika kusimamia na
kuimarisha haki za binadamu kuanzia ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.
Amesema Mhe. Rais Samia amefanikiwa kusimamia haki za
binadamu kwa kuimarisha usawa wa kijinsia nchini, kuimarishaupatikanaji wa
huduma za afya na elimu kwa wasichana, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kupambana
na ukatili wa kijinsia, kuimarisha demokrasia na maridhiano, uhuru wa kutoa
maoni na uhuru wa vyombo vya habari.
Ameongeza kusema ni bahati ya pekee kwa Afrika kuadhimisha
miaka 20 ya Itifaki ya Maputo ya Haki za Wanawake kwenye ardhi ambayo Rais wake
ndiye mwanamke pekee mwenye wadhifa huo wa juu barani humo.
“Hakuna namna bora ya kusherehekea miaka 20 ya Itifaki ya
Maputo ya Haki za Wanawake zaidi ya kusherehekea hapa Tanzania ambapo
Kiongozi wa nchi ndiye Rais pekee
mwanamke barani Afrika. Tuna kila sababu ya kumtunuku tuzo hii siyo tu kwa
sababu ni mwanamke bali pia ni kutokana na hatua kubwa za maendeleo alizopiga
na mchango wake kwenye masuala ya haki za binadamu nchini kwake na kwenye
medani za kimataifa,” amesisitiza Mhe. Sallah-Njie
Amesema nafasi ya Rais Samia ambaye anasismama kama balozi
wa usawa wa kijinsia duniani ni chachu na mfano wa kuigwa kwa wanawake na
wasichana wa Afrika katika kuwahamasisha na kuwatia moyo katika kufanyia kazi
ndoto zao kwa kushinda vikwazo mbalimbali na kwamba wana uwezo wa kushika nafasi
kubwa na za juu za uongozi.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mhe. Balozi Dkt. Chana ameishukuru Tume hiyo
kwa kumtunuku tuzo Mhe. Rais Dkt. Samia na kumuelezea Mhe. Rais kama mwanamke
kiongozi shujaa, mtetezi wa haki za binadamu na watu, mchapakazi na mtoto wa
Afrika ambaye ni mwelewa na ameleta maendeleo nchini.
Amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini
ya Mhe. Rais Dkt. Samia kumekuwa na kasi kubwa katika kuleta maendeleo na
kuwezesha mifumo ya upatikanaji haki kwenye Nyanja mbalimbali ikiwemo utoaji wa
haki huru, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kuabudu, uhakika wa chakula,
kuwawezesha vijana kujiajiri, uwezeshaji wanawake na kuanzishwa kwa mpango wa
msaada wa kisheria wa Dkt. Samia.
Pia amesema katika kipindi hiki cha awamu ya sita ya Mhe.
Dkt. Samia idadi ya wanawake katika vyombo vya utoaji maamuzi ikiwemo Mahakama,
Bunge na Serikalini kwa ujumla imeongezeka.
“Mhe. Dkt. Samia mara baada ya kuingia madarakani alianzisha
falsafa ya R4 kwa maana ya maridhiano na upatanishi, ustahimilivu, mageuzi na
ujenzi mpya. Utaratibu wenye lengo la kustawisha na kudumisha amani, umoja,
undugu na maridhiano kwa wananchi ili kuchocea maendeleo,” amesema Mhe. Balozi
Chana.
Comments
Post a Comment