TANZANIA YAPONGEZWA KWA KUWEKA MIFUMO SHIRIKISHI KATIKA KUIMARISHA HAKI ZA BINADAMU NA WATU
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe, Mathew Mwaimu( Jaji Mstaafu ) akizungumza kwenye kikao cha 77 cha Tume ya Haki za binadamu na watu Oktoba 23,2023 Arusha.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na.
Lusajo Mwakabuku- WKS Arusha
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora nchini, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu ameipongeza
Serikali ya Tanzania kwa kutengeneza mifumo shirikishi yenye lengo la kukuza na
kuimarisha haki za binadamu na watu nchini.
Mhe. Jaji Mwaimu ametoa
pongezi hizo tarehe 23 Oktoba 2023 wakati akihutubia wajumbe wa Kikao cha
Kawaida cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachoendelea
jijini Arusha.
Mhe. Jaji Mwaimu amesema kuwa
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanikiwa kuweka mifumo shirikishi
inayowezesha wadau mbalimbali kujadili mambo muhimu ya kitaifa ikiwemo ya
kisiasa, kijamii na kiuchumi ikiwa ni jitihada za Serikali za kuendelea
kuimarisha na kuboresha usimamizi wa haki za binadamu na watu.
Akizitaja hatua za Serikali zinazodhihirisha mwenendo
mzuri wa kuimarika na kustawi kwa haki za bianadamu na Watu nchini kuwa ni
pamoja na kuwekwa mfumo shirikishi wa kujadili mambo muhimu ya Kitaifa na
kuimarika kwa demokrasia ambapo Mhe. Rais Samia aliunda Kamati Maalum kwa ajili
ya kutathmini mwenendo mzima wa masuala ya siasa nchini.
“Tunapenda katika mkutano huu kuweka
msisitizo katika masuala machache ambayo Tume imeona kwamba yana mwelekeo
chanya na yamejipambanua kutokana na umuhimu wake. Kwanza ni hatua ya Serikali
ya Tanzania ya kuweka mfumo shirikishi wa kujadili mambo muhimu ya kitaifa.
Mfano hivi karibuni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na
Vyama vya Siasa nchini walikaa pamoja jijini Dar es Salaam kujadili taarifa ya
kamati Maalum iliyoundwa ba Mhe. Rais Dkt. Samia kwa ajili ya kukuza mwenendo
mzima wa masuala ya siasa ikiwemo demokrasia ya Vyama Vingi.
Pia amepongeza hatua ya
kuzinduliwa kwa Kampeni ya miaka mitatu ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria
ambayo mpaka sasa imetekelezwa kwenye mikoa mitano na kuwafikia zaidi ya
wananchi 2,870 waliopo kwenye maeneo 39 ya vizuizi na zaidi ya wananchi 361,740
waliopo uraiani wamehudumiwa kwa ukamilifu na kufaidika.
Amesema, miongoni mwa
waliofaidika na Kampeni hii ni wahamiaji raia wa Ethiopia zaidi ya 80 ambao
walirejeshwa nchini kwao baada ya kuwa vizuizini kwa changamoto za uhamiaji.
Mhe. Jaji Mstaafu Mwaimu pia
aliutaja mchakato ulioanzishwa na Mhe. Rais Dkt. Samia wa kupitia upya mfumo wa
Taasisi zinazoshughulikia masuala ya Haki Jinai kuwa ni wenye tija kubwa na wa kuigwa kwenye kuimarisha Nyanja za haki za binadamu na watu nchini.
“Tume imeona suala la Mhe.
Rais Dkt. Samia la kuanzisha mchakato wa kupitia upya mfumo wa taasisi
zinazoshughulikia masuala ya haki jinai kuwa ni jambo kubwa na lenye tija.
Mchakato huu ambao unalenga kufanya mapitio ya mnyororo mzima wa haki jinai kwa
kushughulikia dosari za upatikanaji wa haki za binadamu utaleta tija na
kuimarisha haki za binadamu hapa nchini pale utakapokamilika,” alisisitiza Mhe.
Jaji Mwaimu.
Pia Tume hiyo imepongeza
utayari wa Serikali wa kuanza kuandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Biashara na Haki
za Binadamu ambao ukikamilika utawezesha kuingiza katika mfumo Kanuni za Umoja
wa Mataifa za masuala ya Haki za Binadamu na Biashara na kuwahakikishia
Watanzania kufanya shughuli za biashara kwa namna inayozingatia na kuhifadhi
haki za binadamu.
Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora ni Idara huru ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2001 ambayo pamoja
na mambo mengine husimamia utekelezaji wa haki za binadamu na watu nchini.
Kikao cha Kawaida cha 77 cha
Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kilifunguliwa rasmi tarehe 20 Oktoba
2023 na kinatarajiwa kumalizika tarehe 09 Novemba, 2023.
Comments
Post a Comment