Wananchi Tumieni Kikamilifu Fursa Mbalimbali Zinazobuniwa na Serikali – Dkt. Chana
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana akihutubia katika uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano Mkoani Kigoma, 03 Oktoba, 2023.
Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana akitoa vyeti vya kuzaliwa kwa
baadhi ya watoto waliohudumiwa wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano Mkoani
Kigoma, 03 Oktoba, 2023.
Na
William Mabusi – WKS
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt.
Pindi Chana ametoa wito kwa wananchi kutumia kikamilifu fursa mbalimbali
zinazobuniwa na Serikali na ambazo zinaigharimu Serikali fedha nyingi.
Balozi Dkt. Chana ametoa wito huo wakati akihutubia
mamia ya wananchi waliofurika kwenye uwanja wa Mwanga Community Centre wakati
wa uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano Mkoani
Kigoma, tarehe 03 Oktoba, 2023.
Mpango huo ambao unasogeza huduma ya usajili
karibu na maeneo ya makazi yaani katika Ofisi za Watendaji Kata na katika Vituo
vya Tiba unatekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini
(RITA) kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Maendeleo wenye lengo la
kutambua haki za watoto, kuboresha hali ya usajili wa vizazi nchini kwa kupanua
wigo wa upatikanaji wa huduma kwa maendeleo ya Taifa.
Pamoja na usajili wa watoto Dkt. Chana akatoa
wito kwa watu wazima kusajili na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa, “na sasa RITA
imerahisisha upatikanaji wa huduma kwani waweza kutuma maombi ya huduma
kidijitali popote ulipo kwa kutumia
mfumo wa eRITA. Serikali inawekeza fedha nyingi kubuni mipango hivyo wananchi
tutumieni fursa hizo kikamilifu.”
Mpango huo umezinduliwa nchini mwezi Juni mwaka
2013 na hadi sasa zaidi wa watoto 8,646,324 wamesajiliwa na kupata vyeti vya
kuzaliwa kwenye mikoa 24 ambayo mpango huu umetekelezwa. Katika kutekeleza
mpango huo mkoani Kigoma jumla ya watoto 396,182 wanatarajiwa kusajiliwa na
kupata vyeti vya kuzaliwa. Mhe. Chana akatoa wito kwa kaya zenye watoto walio
chini ya miaka mitano kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hilo.
Comments
Post a Comment