DKT. CHANA AIPONGEZA NPS KWA UTENDAJI KAZI
Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akiwa kwenye picha ya pamoja na Menejimenti ya Ofisi
ya Taifa ya Mashtaka, tarehe 02 Novemba, 2023 Jijini Dodoma.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi
Dkt. Pindi Chana akiongea na watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, tarehe 02
Novemba, 2023 Jijini Dodoma.
Naibu Waziri
wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul akimkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria
kuongea na watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, tarehe 02 Novemba, 2023
Jijini Dodoma.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na William Mabusi – WKS Dodoma
Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) ametembelea Ofisi ya Taifa
ya Mashtaka (NPS) na kupokea tarifa ya utekelezaji ya mwaka wa fedha 2022/23 na
kuipongeza kwa utekelezaji wa majukumu yake ya usimamiaji haki nchini.
Dkt. Chana
akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (Mb),
SACP Neema Mwanga aliyemwakilisha Katibu Mkuu amekutana na Menejimenti na
watumishi wa ofisi ya NPS tarehe 02 Novemba, 2023 kwenye ofisi za Taasisi hiyo
Jijini Dodoma.
“Tanzania si tu ina Mahakama
lakini pia
mtu ana uhakika wa kupatikana kwa haki yake na kwa wakati kwani tunashuhudia
wenyewe kuongezeka kwa kasi ya kutoa maamuzi ya mashauri mbalimbali kwenye
Mahakama zetu,” alisema Dkt. Chana.
Akiongelea
kuhusu ushirikiano mzuri uliopo kati ya NPS na Ofisi zingine za Kikanda na
Kimataifa ameitaka ofisi hiyo na Taasisi zingine za Wizara kutumia mwonekano wa
nchi yetu kimataifa wa kusimamia na kuimarisha haki za binadamu kutafuta Wadau
wengi wa Maendeleo watakaosaidia kufadhili utekelezaji wa miradi mbalimbali.
“Pamoja na
jitihada za Serikali za kukabiliana na changamoto mbalimbali kwenye Taasisi
zake bado natoa wito tuongeze ushirikiano na Wadau wa Maendeleo. Kuna baadhi ya
nchi vipaumbele vyao ni haki za binadamu hivyo kwa kuwa tunasifika kama nchi
inayozingatia utawala wa sheria, nchi kama hizo ndizo za kushirikiana nazo.
Ushirikiano huo utatuwezesha kukabiliana na changamoto kama upungufu wa
vitendea kazi, mafunzo ya teknolojia kwenye sekta mbalimbali na utekelezaji wa
miradi ya maendeleo.” Alisema.
Aidha, Dkt.
Chana ameunga mkono uamuzi wa wafungwa kuhusishwa kwenye shughuli za uzalishaji
katika kilimo na shughuli zingine za maendeleo, “Magereza yawe na mashamba kwa
ajili ya kilimo ili tusije kuwa tunachukua pesa ya mtenda haki kwenda kulisha
mhalifu, na kila mnapowatembelea ‘maana ni jukumu lenu pia’ wakumbusheni kuwa
wao ni watanzania wenzetu na kuwahimiza kuacha uhalifu ili wawe raia wema
watakapomaliza vifungo vyao.”
Awali
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji, Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Bw. Sylvester
Mwakitalu ameshukuru na kupongeza lengo la Serikali la kufungua ofisi za
Mashtaka katika kila Wilaya nchini ambapo hadi sasa bado Wilaya 47. Aidha,
amesema NPS kama kiungo kikubwa katika mnyororo wa haki jinai wataendelea
kushirikiana na vyombo vingine vya uchunguzi kusimamia haki na wataendelea
kusimamia mashirikiano mazuri ya kikanda na kimataifa kwenye masuala ya jinai.
Comments
Post a Comment