SISI TUNA UHITAJI LAKINI WATOTO HAWA WANA UHITAJI ZAIDI: MAKONDO
Katibu Mkuu
wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo na watumishi wa Wizara kwenye
picha ya pamoja na wafanyakazi wa Kituo cha Safina Street Network, tarehe 04
Novemba, 2023 Jijini Dodoma.
Watoto
wanaolelewa katika Kituo cha Safina Street Network kilichopo maeneo ya Ntyuka
wakipata chakula walichoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria, tarehe 04
Novemba, 2023 Jijini Dodoma.
Na
William Mabusi – WKS Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na
Sheria Bi. Mary Makondo amesema Watoto wanaolelewa kwenye vituo mbalimbali vya
yatima na wanaotoka katika mazingira hatarishi hapa nchini wana uhitaji mkubwa
na changamoto nyingi kulinganisha na watu wengine, na kutoa wito kwa jamii
kuendelea kuwakumbuka watoto hao mara kwa mara kwa kuwapelekea mahitaji
mbalimbali ili kuwatia moyo kwenye maisha wanayopitia.
Bi. Makondo
ameyasema hayo wakati yeye na watumishi wa Wizara hiyo walipotembelea kituo cha
kulelea watoto wanaotoka kwenye mazingira hatarishi kiitwacho Safina Street
Network kilichopo maeneo ya Ntyuka, tarehe 04 Novemba, 2023 Jijini Dodoma.
Katika tukio
hilo Bi. Makondo na watumishi wa Wizara hiyo wameshiriki nao chakula cha mchana,
kuimba nao nyimbo za kumtukuza Mungu kisha kuwakabidhi vitu mbalimbali vikiwemo
sukari, chumvi, viatu vya wazi, nguo, sabuni unga na
mafuta ya kupikia huku akiwataka watoto hao kushika mahusia ya Walimu
wao na kusoma na kulishika Neno la Mungu.
“Sote ni
wahitaji lakini Watoto hawa wana uhitaji zaidi, sote tuna changamoto lakini
watoto hawa wana changamoto zaidi, sote tunashida lakini watoto hawa wanashida
zaidi. Badhi ya watoto hawa hawana wazazi na wengine wana wazazi lakini
wamewatelekeza, ni wajibu wa jamii kuwa nao na kuwafanya wenzetu,” alisema.
Kuhusu
changamoto zozote za kisheria kwa watoto hao Bi. Makondo alisema,
“tunawachukulia ninyi kama ndugu zetu, msisite kutwambia changamoto zenu
zinazohusu ukosefu wa haki, unyanyasaji wa kijinsia au pale mtakapohitaji
huduma za Serikali kwenye uhitaji wa sheria. Niwakumbushe kuwa Wizara ya Katiba
na Sheria inatekeleza kampeni kubwa ya Msaada wa Sheria ya Mama Samia yenye
lengo kutoa elimu na huduma ya sheria ili watanzani hasa wanyonge wapate haki.”
Naye Mratibu
wa Kituo hicho chenye takribani watoto hamsini wa umri chini ya miaka saba hadi
ishirini na tano wa kike na wa kiume Bw. Ebenezer Eliawira Ayo ameshukuru sana
ujio huo akisema “matukio kama haya ya wageni kuwatembelea huwatia sana watoto
moyo, huwapa faraja na huwa ni ukumbusho kuwa huko nje kuna maisha na kuna watu
wanawajali, wanawapenda na wanawaombea.”
Mnufaika wa
kituo hicho David Shaban anashukuru jinsi kituo hicho kilivyomtoa kwenye maisha
ya mtaani, kimemlea na sasa anakitumikia kituo hicho kama mfanyakazi baada ya
kuhitima elimu yake.
Comments
Post a Comment