TANZANIA IMESAJILI NA KUTOA VYETI VYA KUZALIWA KWA WATOTO ZAIDI YA MILIONI NANE




Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri chini ya miaka mitano, Desemba 08, 2023 katika viwanja vya Mbagala Zakhiem Jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu Wizira ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri chini ya miaka mitano, Desemba 08, 2023 katika viwanja vya Mbagala Zakhiem Jijini Dar es Salaam.



Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizindua Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri chini ya miaka mitano, Desemba 08, 2023 katika viwanja vya Mbagala Zakhiem Jijini Dar es Salaam.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Na Lusajo Mwakabuku - DSM

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa Watoto zaidi ya milioni 8.8 wamesajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara kupitia Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri chini ya miaka mitano.

Mhe. Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango leo Desemba 08, 2023 katika viwanja vya Mbagala Zakhiem Jijini Dar es Salaam.

Uzinduzi huu unahitimisha Mikoa 26 ya Tanzania bara ambapo Mkoa wa Dar es Salaam unatarajiwa kusajili jumla ya watoto 248,298 na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa bila ya malipo kupitia vituo 505 vya usajili ambavyo ni Vituo vya Afya na Ofisi za Watendaji wa Kata.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amesema, mpango huo ulioanza jijini Mbeya mwaka 2013 na kuhitimishwa jijini Dar es Salaam ikiwa ni  jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ambayo imekuwa ikitenga bajeti ya utekelezaji wa majukumu  hayo na  kuhakikisha wananchi wanasogezewa huduma katika maeneo wanakoishi.

Ameongeza kuwa, mpango huo ni mfano wa maboresho kwa kuwa huduma zimesogezwa karibu na wananchi na kutumia teknolojia ya simu za mkononi ambayo inarahisisha upatikanaji wa takwimu za watoto wengi wanaosajiliwa ndani ya muda mfupi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri RITA Dkt. Amina Msengwa amesema kuwa mpango huo ulianzishwa na Serikali kupitia RITA kwa kundi hilo la kimkakati la watoto kwani mipango mingi ya maendeleo hutegemea takwimu sahihi na hivyo kupitia mpango huo utawezesha Serikali kupata takwimu sahihi kwa wakati.

Naye Kabidhi Wasii Mkuu Bw. Frank Kanyusi amesema, Lengo la Mpango huo ni kuongeza kasi ya ya Usajili na kutoa vyeti kwa watoto wa Umri chini ya miaka mitano pamoja na kusogeza huduma kwa wananchi kuanzia ngazi ya Kata.

"Chimbuko la mpango huu ni kasi ndogo ya usajili, Serikali kwa kushirikiana na wadau wakaleta mpango huu ili kuongeza kasi ya usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watanzania wote." Amesema.

Pia, amewashukuru wadau mbalimbali wa Kitaifa na Kimataifa ambao ni Serikali ya Canada, Shirika la kuhudumia watoto duniani UNICEF, Kampuni ya simu za mkononi Tigo na kuahidi kuendelea na ushirikiano katika utoaji wa huduma hiyo kwa wananchi.

 

 


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA