“UNYANYASAJI WA KIJINSIA HAUNA NAFASI KATIKA NCHI YETU” DKT. CHANA
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
akihutubia wakati akifungua Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, tarehe 06
Desemba, 2023 Jijini Dodoma.
Washiriki siku ya kufungua Siku 16 za Kupinga Ukatili wa
Kijinsia, wakimkaribisha ukumbini Mgeni Rasmi Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Balozi Dkt. Pindi Chana tarehe 06 Desemba, 2023 Jijini Dodoma.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi walioshiriki hafla ya kufungua Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, tarehe 06 Desemba, 2023 Jijini Dodoma.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na William Mabusi – WKS Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema Tanzania inaweza kusonga mbele na kushinda
vita dhidi ya Ukatili wa Kijinsia ikiwa wote tutazungumza na kupaza sauti
kupinga Unyanyasaji wa kijinsia huku akiitaka jamii kushiriki kikamilifu katika
kutoa ushahidi wa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia mara inapotakiwa kufanya
hivyo.
Ameziagiza Taasisi za dini na
Wazee wa kimila, Wanahabari na Wadau wa Maendeleo na wananchi wote wawe tayari
kuchukua hatua za maksudi kukomesha ukatili wa kijinsia kwenye jamii zetu
kuanzia familia, makazini kwetu na kwenye jamii zetu kwa ujumla.
Dkt. Chana ameyasema hayo
alipokuwa akifungua Maadhimidho ya siku 16 za Kupinga Ukatili dhidi ya
Kijinsia, tarehe 06 Desemba, 2023 Jijini Dodoma, tukio ambalo limefanyika chuo
Kikuu cha Dodoma.
“Tuwaamini wenzetu pale
wanapotuambia wananyanyaswa, tuwasikilize na tuwasaidie, na hata tukiwa
nyumbani tuwe wasikivu kwa watoto, wakituambia wanafanyiwa vitendo vya ukatili
wa kijinsia tufuatilie kwa ukaribu na kuchukua hatua za kisheria, tuache
kumaliza masuala ya ukatili kifamilia kwani watendaji wataendelea kufanya
vitendo hivyo.” Alisema.
Dkt. Chana ameongeza kuwa
“ukatili wa kijinsia ni moja ya changamoto kubwa inayorudisha nyuma juhudi za
kutambua usawa wa binadamu na utu wa mwanamke katika dunia ya leo, ni zao la
mtizamo usio sahihi uliojengeka kwenye mila na desturi katika jamii
unaomchukulia mwanamke kama mali ya mwanaume na kwamba ni kiumbe aliyeumbwa kutekeleza
utashi wa mwanaume.”
Wakati Tanzania ikifanya
Maadhimisho ya kimataifa ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia takwimu
zinaonesha kuwepo kwa ongezeko la matukio ya ukatili huo hapa nchini. Ongezeko
hilo linatokana na sababu mbalimbali ikiwemo jamii kuwa na uelewa zaidi juu ya
madhara yatokanayo na ukatili wa kijinsia na kutoa taarifa za matukio ya
ukatili huo katika Madawati ya Jinsia.
Sababu zingine ni mmomonyoko wa
maadili, hali ngumu ya maisha ambayo huleta msongo wa mawazo kwa baadhi ya watu
na kujikuta wakitenda matukio hayo. Sababu nyingine ni mila na tamaduni kandamizi, kushamiri kwa
mfumo dume katika jamii zetu, matumizi
mabaya ya teknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakisababisha
vijana kufanya vitendo vya kikatili hasa ubakaji wa watoto na wanawake lakini
pia kulawiti.
Katika kukabiliana na vitendo vya
ukatili wa kijinsia nchini Dkt. Chana amesema Serikali inaendelea kuimarisha
mifumo ya upatikanaji haki kwa wananchi hususan wanawake, watoto na makundi
maalum ikiwa ni pamoja na kutunga sheria mbalimbali, kufanya maboresho ya mara
kwa mara ya sheria, kanuni, miongozo na hata sera zinazosimamia usawa na ulinzi
wa makundi mbalimbali.
Aidha, Serikali inayo mikakati
mbalimbali ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia
akiitaja moja ya mikakati hiyo kuwa ni Kampeni Kabambe ya Huduma za Msaada wa
Kisheria iitwayo Mama Samia Legal Aid Camapign ambayo inatekelezwa na Wizara ya
Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Wadau wa masuala ya upatikanaji haki hapa
nchini.
Amevipongeza vyombo vya utoaji haki kuhakikisha washukiwa wote wa vitendo vya ukatili wa kijinsia wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, kushughulikia mashauri kwa wakati na hivyo kesi kuhitimishwa ndani ya muda mfupi.
Dkt. Chana amelishukuru Shirika
la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), kwa kushirikiana na Wizara na Chuo Kikuu cha
Dodoma katika kuandaa maadhimisho hayo. Amemtaka Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma
Prof. Lughano Kusiluka na Amidi wa Shule ya Sheria Dkt. Ines Kajiru kuendelea
kuwajenga wanafunzi wao katika misingi ya kuwa mabalozi wema wa masuala ya
ukatili wa kijinsia,
Aidha, ameaomba Wadau wa
Maendeleo na Mashirika yanayotetea haki za wanawake na watoto kuongeza
mashirikiano ya muda mrefu na usaidizi katika kuunga juhudi za Serikali katika
kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia miongoni mwa jamii huku akiyataka
mashirika hayo kujikita zaidi katika maeneo ya pembezoni kwani kule ndipo
kwenye changamoto zaidi kutokana na ukweli kwamba, elimu ya masuala haya bado
haijafika vya kutosha kwahiyo jamii bado inaamini katika mila na desturi.
Comments
Post a Comment