KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA MAJIBU YA SERIKALI
Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
akichangia kujibu hoja kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya ya Bunge ya
Utawala, Katiba na Sheria na Wizara, tarehe 23 Januari, 2024 Kumbi za Bunge.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo
(kushoto), Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi
(katikati) wakifuatilia kwa makini majibu ya Serikali kuhusu hoja za Bunge,
tarehe 23 Januari, 2024 Kumbi za Bunge.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na William Mabusi - WKS Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria
ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Florent Kyombo imeridhishwa na
majibu ya hoja zote kumi zilizowasilishwa na Bunge kwa Wizara ya Katiba na
Sheria mwezi Februari, 2023.
Kikao cha Kamati hiyo kimefanyika tarehe 23 Januari, 2024 kwenye
kumbi za Bunge ambapo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
akiongozana na Katibu Mkuu wa Wizara Bi. Mary Makondo, baadhi ya Wakuu wa
Taasisi zilizo chini ya Wizara na Wataalamu alitoa majibu ya hoja hizo.
Hoja zilizowasilishwa na Bunge ni pamoja na Miswada
inayosomwa Bungeni kwa lugha ya Kiswahili itafsiriwe kwa lugha ya Kiingereza
ili kuwasaidia watumiaji wasiojua lugha ya Kiswahili, Serikali iharakishe
mchakato wa kusanifu programu ya kutafsiri mwenendo wa mashauri na hukumu za Mahakama
kutoka katika Lugha ya Kiingereza kwenda katika Lugha ya Kiswahili ili
kurahisisha upatikanaji wa haki kwa haraka, Serikali kutilia mkazo elimu kwa
wadau na wananchi kuhusu umuhimu na faida za utatuzi wa migogoro kwa njia
mbadala, miongoni mwa zingine.
Akisoma majibu ya hoja hizo kwa niaba ya Waziri wa Katiba na
Sheria, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Bw. Mbaraka Stambuli amesema tangu
kufanyika kwa mabadiliko ya Tafsiri ya Sheria Sura ya 1, Kiswahili kilifanywa
kuwa lugha ya kutungia sheria. Katika kujibu hoja ya Bunge, kifungu hicho
kimefanyiwa tena marekebisho kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali
Na. 3 ya mwaka 2023 ili kuitaka Serikali kuhakikisha kuwa Sheria yoyote
inayotungwa kwa lugha ya Kiswahili inatafsiriwa kwenda Lugha ya Kiingereza
ndani ya siku 90 baada ya kuanza kutumika.
Bw. Stambuli ameendelea kusema kuwa ili kurahisisha zoezi la
kutafsiri hukumu na kumbukumbu za kimahahakama kwa lugha ya Kiswahili, Mahakama
imeanza kutumia Mfumo wa Kunukuu na Kutafsiri Kumbukumbu za Kimahakama
(Translation and Transcription System – TTS), hatua itakayoongeza kasi ya
maamuzi na mienendo ya kimahakama kupatikana kwa lugha ya Kiswahili.
Aidha, Serikali inaendelea na uhakiki wa Sheria 258
zilizotafsiriwa katika lugha ya Kiswahili ili zitangazwe katika Gazeti la
Serikali na kuanza kutumika. Pia, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali
imepanga kutafsiri sheria kuu 188 zilizobakia.
Katika kuongeza ufanisi wa utekekelezaji wa majukumu ya Ofisi
ya Taifa ya Mashtaka ili kuharakisha
kukamilika kwa kesi za jinai, kufanikisha zoezi la kutenganisha shughuli za
mashataka na upelelezi, Serikali imeandaa Mpango Kabambe wa miaka mitano
(2023/2024 - 2027/2028) ambao unahusisha ujenzi wa majengo ya ofisi,
upatikanaji wa vitendea kazi, ununuzi wa vifaa vya TEHAMA na magari.
Katika kufanikisha zoezi la utenganishaji wa shughuli za
upelelezi na mshtaka Ofisi mpya za wilaya 50 zimefunguliwa na hivyo kufanya
kuwa na jumla ya Ofisi 92 za Wilaya na kubakiwa na wilaya 47 ambazo hazina
Ofisi.
Akijibu hoja ya utoaji wa elimu kwa wadau na wananchi kuhusu
umuhimu na faida za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala. Amesema Wizara kwa
kushirikiana na Taasisi zilizo chini ya Wizara imekuwa ikitumia matukio ya
kitaifa kama vile Wiki ya Sheria, Wiki ya Msaada wa Kisheria, Kampeni ya Msaada
wa Kisheria ya Mama Samia, Maonesho ya Wakulima ya Kitaifa na Siku ya Maadili
na Haki za Binadamu Kitaifa kila mwaka kutoa elimu ya sheria pamoja na utatuzi
wa migogoro kwa njia mbadala kwa umma na wadau wengine.
Aidha, Wizara ya Katiba na Sheria imefanya marekebisho ya
Sheria ya Usuluhishi Sura ya 15 ya mwaka 2020 kupitia Sheria ya Marekebisho ya
Sheria ya Sekta ya Sheria ya mwaka 2023 kwa madhumuni ya kuimarisha mfumo wa
usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala nchini.
Akihitimisha majibu ya hoja hizo Dkt. Chana amesema Wizara ya
Katiba na Sheria pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara itaendelea kutekeleza
maoni na mapendekezo ya Kamati kadri inavyoelekezwa kwa maslahi mapana ya nchi.
Comments
Post a Comment