MAHAKAMA IJIANDAE KUKABILIANA NA WIMBI LA KESI ZA AKILI BANDIA (ARTIFICIAL INTELLIGENCE)
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Tulia Ackson akihutubia kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya
Sheria yaliyofanyika Kitaifa Jijini Dodoma tarehe 27 Januari, 2024
Bw. Emmanuel Mbega Wakili wa Serikali
Mkuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria akitoa maelezo kwa Mhe. Dkt. Tulia
Ackson kwenye Banda la Wizara, tarehe 27 Januari, 2024 kwenye Viwanja vya
Nyerere Square Jijini Dodoma.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na William Mabusi – WKS Dodoma.
Spika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani
Dkt. Tulia Ackson ameitaka Mahakama ya Tanzania kujiandaa kukabiliana na
waathirika wa matumizi ya akili bandia wakati ikiendelea kuboresha matumizi ya
TEHAMA katika kutoa haki.
Dkt. Tulia
ameyasema hayo alipokuwa akihutubia kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya
Sheria yaliyofanyika Kitaifa Jijini Dodoma tarehe 27 Januari, 2024 ambapo yeye
alikuwa Mgeni Rasmi. Kabla ya uzinduzi huo Dkt. Tulia aliongoza matembezi
yaliyoanzia Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kuishia Viwanja vya
Nyerere Square.
“Kwa kuwa
sehemu kubwa ya mfumo unatumia akili bandia naiona hatari ya wadanganyifu kutumia
teknolojia hiyo kugombanisha watu au kupotosha nia nzuri ambayo tunaitamani kwa
matumizi ya akili bandia. Hivyo naomba mjiandae kukabiliana na kesi za
waathiriwa na matumizi ya akili bandia. Kwani kwa kutumia akili bandia mtu
anaweza kufanywa kafanya tukio na kumbe kiuhalisia siye, mdanganyifu anaweza
kutumia sauti ya mtu anayefahamika kusikika kwenye maneno ambayo anataka
yamfikie mtu fulani au umma fulani.” Alisema baada ya kuzindua mfumo wa Unukuzi
na Tafsiri wa Mienendo ya Mashauri (Transcription and Translation- Software –
TTS).
Awali
akimkaribisha Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, alisema mfumo wa Unukuzi na
Tafsiri wa Mienendo ya Mashauri unatumia akili bandia au mnemba (Artificial
intelligence) na umefundishwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza cha kisheria na kimahakama
kwa mazingira ya Tanzania ili usaidie kufanya unukuzi (transcription) na pia
kutafsiri (translation) katika lugha ya Kiswahili au Kiingereza.
Mfumo huo unawapunguzia
Majaji na Mahakimu kazi kubwa waliyokuwa wanaifanya ya kuandika kwa mkono
mienendo ya mashauri na kisha kuchapwa na Makatibu Mahsusi na hivyo
kupelekea wananchi kupata haki kwa wakati hasa wanapokuwa wanataka kukata rufaa.
Mfumo wa TTS
umeshafungwa na kuanza kutumika kwa awamu ya kwanza katika Vituo Jumuishi vya
Utoaji Haki vya Arusha, Dodoma, Mwanza Kinondoni, Temeke na Morogoro, Mahakama
Kuu Dar es Salaam, Bukoba na Musoma.
Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana hakuweza kushiriki ufunguzi wa
maadhimisho hayo kwa kuwa yuko kwenye majukumu mengine nje ya Dodoma.
Maadhimisho
ya Wiki ya Sheria yameanza tangu tarehe 24 Januari 2024 kwenye Viwanja vya
Nyerere Square ambapo Wadau wa utoaji haki wanatoa elimu ya sheria, msaada wa
kisheria na kuzungumza na wananchi mambo mbalimbali yahusuyo umuhimu wa haki
kama kigezo muhimu cha ustawi wa taifa. Maadhimisho ya Wiki ya Sheria
yatahitimishwa tarehe 01 Februari, 2024.
Comments
Post a Comment