SERIKALI INA DHAMIRA YA DHATI YA KUANZISHWA KWA MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA – WAZIRI CHANA
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Balozi Dkt. Pindi Chana na viongozi pamoja na wananchi wa kijiji cha Nkomamanga
wakiimba na kumfurahia Rais Samia baada ya kupata taarifa za mradi wa Liganga
na Mchuchuma. 05/01/2024
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Balozi Dkt. Pindi Chana akiongea na wananchi wa kijiji cha Nkomang’ombe
wilayani Ludewa ambapo mradi wa Mchuchuma unatekelezwa, 05/01/2024.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri Asili na Maliasilia za Nchi Kamishna Bi, Neema Mwanga akitoa taarifa ya kisheria juu ya utekelezwaji wa mradi wa Liganga na Mchuchuma, 05/01/2024.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na Lusajo Mwakabuku – WKS Njombe
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha mradi huu
unatekelezwa mapema iwezekanavyo ndio maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha malipo ya fidia kwa wananchi wote
waliopisha eneo la utekelezaji wa mradi mkubwa wa Liganga na Mchuchuma Wilayani
Ludewa Mkoani Njombe.
Waziri Chana ameyasema hayo
tarehe 05/01/2023 akiwa katika Kijiji cha Nkomang’ombe kilichopo katika wilaya
ya Ludewa Mkoani Njombe akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani humo
akitekeleza jukumu lake la kusimamia misingi iliyowekwa na Sheria Sura 449 na
450 yenye lengo la kuhakikisha uwekezaji katika uvunaji na matumizi ya utajiri
asili na maliasilia za nchi unatekelezwa kwa namna ambayo inainua hali ya
wananchi kiuchumi na kuongeza pato la Taifa.
“Lengo la ziara hii ni kufuatilia
utekelezaji wa Sheria hizi katika miradi ya Liganga na Mchuchuma. Aidha, Sheria
hizi zinaweka misingi ya kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Ludewa na waliopo
karibu na maeneo ya miradi hii wananufaika na fursa zinazopatikana katika
uwekezaji wa rasilimali za Taifa. Kwa mfano, ni matarajio ya Serikali kuwa,
uwekezaji wa miradi ya namna hii itatoa ajira kwa watanzania, itatoa fursa ya
watanzania kusambaza zabuni kwa watanzania na kuwapa mafunzo yanayolenga
kuhuisha teknolojia kwani kwa kufanya hivyo ndiyo utekelezaji wa misingi
iliyowekwa na Sheria zetu.”alisema
Waziri Chana.
Aidha, Waziri Chana amesema kuwa
pamoja na kwamba mradi huo una historia ndefu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha nia ya wazi ya
kutekeleza mradi huo kwa kutoa kiasi hicho cha fedha ili miradi hiyo
inaojumuisha uchimbaji wa chuma Liganga pamoja na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma
ianze kazi mara moja baada ya maafikiano ya kimikataba kufikiwa.
Waziri Chana pia akatumia nafasi
ya ziara yake ya siku mbili kuongea na wananchi wa vijiji vya Nkomang’ombe na
Mundindi ambapo miradi hiyo inatekelezwa na kuwataka wawaandae vijana wao
katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kielimu, uwekezaji mdogo mdogo na ujuzi
ili mradi utapoanza basi waitumie nafasi hiyo vizuri kuhakikisha wanufaika wa
kwanza wanakuwa wananchi wa maeneo husika.
Akiongelea hatua mbalimbali za
kitaalam ambazo mradi huo umepitia, Meneja wa Mradi wa Liganga na Mchuchuma
kutoka NDC Dkt. Witness Ishuza alisema “Mwaka 2013 Tafiti ya Makaa za mawe
pamoja na Chuma zilifanyika, kwa kipindi hicho na kugundua kwamba kuna tani milioni 428 za
Makaa ya mawe katika eneo la ukubwa wa mraba 30 ambazo zinaweza kuchimbwa kwa
miaka zaidi ya 140 na Chuma ambacho ni
zaidi ya tani milioni 126 ambacho kinaweza kuchimbwa kwa miaka 58.”
Naye Mwenyekiti wa CCM katika
Wilaya ya Ludewa amesema Rais Samia amefanya jambo kubwa kwani ametekeleza
jambo ambalo ni kiu kubwa ya wananchi na kwamba Taifa litakwenda kusonga mbele
kwani mradi huo unakwenda kubadilisha uchumi wa Taifa letu na kupunguza gharama
kubwa zinazotumika katika kuagiza chuma kutoka nje tena kwa kutumia fedha za
kigeni, hivi viwanda vyote vya nondo, viwanda vya umeme, viwanda vya mabati,
vitatumia chuma chetu.
Rafael Memba mmoja wa wanufaika
wa fidia ya kupisha mradi wa Liganga na Mchuchuma na mkazi wa Kijiji cha
Nkomang’ombe alimshukuru Mhe. Rais Samia kwa kutimiza ahadi yake ya kulipa
fidia licha ya kusubiri muda mrefu na pia akaiomba Serikali kuhakikisha
taratibu mbalimbali zinazokwamisha mradi huo kuanza zinakalika kwa haraka ili
mradi uweze kufanyika kwa haraka na kuleta mafanikio kwao binafsi na kwa Taifa
kwa ujumla.
Comments
Post a Comment