SERIKALI ITAENDELEA KULINDA NA KUKUZA UPATIKANAJI HAKI – DKT. CHANA
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Balozi Dkt. Pindi Chana na Meza Kuu kwenye picha ya pamoja na sehemu ya
watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria, 10/01/2024 Singida.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Balozi Dkt. Pindi Chana akihutubia wakati anazindua utekelezaji wa Kampeni ya
Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, 10/01/2024 Mkoani Singida
Na William Mabusi –
WKS Singida
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali itaendelea kulinda na kukuza
upatikanaji haki nchini kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya kisera ya Kitaifa
ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa
na usawa mbele ya sheria, wananchi wanalindwa na wanapata haki kupitia vyombo vya haki.
Dkt. Chana ameyasema hayo Mkoani
Singida alipokuwa anazindua utekelezaji wa Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa
Kisheria ijulikanayo kama Mama Samia Legal Aid Campaign iliyoanza kutekelezwa
mkoani humo leo tarehe 10 Januari, 2024.
“Lengo la utekelezaji wa kampeni
hii ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada
wa kisheria nchini ambayo ni utekelezaji wa Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania ibara ya 8 (1) (b) na Ibara ya 13 (1) zinazoweka msingi wa haki na
usawa na ustawi wa wananchi.”
Ameyataja mafaniko makubwa
yaliyopatikana tangu kuanza kutekelezwa kwa kampeni hiyo mwezi Aprili 2023 hadi
kufikia Oktoba, 2023 ambapo jumla ya mikoa mitano imeshatembelewa, kuwa ni pamoja na jumla ya migogoro 6,365 iliyohusu masuala ya ardhi, ndoa, mirathi na matunzo ya
watoto ilipokelewa ambapo kati ya hiyo
migogoro 488 ilitatuliwa na
kuhitimishwa. Migogoro 5,877 inaendelea kushughulikiwa katika mamlaka mbalimbali za kimahakama na kiutawala na
Wizara kupitia Waratibu na Wasajili wa mikoa na wilaya imeendelea kufuatilia
utekelezaji wake.
Aidha, wananchi 2,055
(Wanaume1,035 Wanawake 1,020) walisajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa
kupitia Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu – RITA, kumekuwepo na ongezeko la uelewa na uwajibikaji wa Watendaji wa
Vijiji, Kata, Halmashauri, Viongozi wa kidini na kimila, Wanafunzi na Walimu wa
Shule za Msingi na Sekondari katika kuwahudumia wananchi na kuwasaidia kudai na
kupata haki zao baada ya kujengewa uwezo katika masuala mbalimbali ya sheria,
haki za binadamu na utawala bora.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria inatokana na adhma ya Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
kuhakikisha kwamba kila mwananchi
anafahamu masuala ya kisheria ikiwemo haki na wajibu wake na kwamba kila
mwananchi anaifikia haki na wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili
waweze kufikia haki kupitia huduma za msaada wa kisheria.
Kupitia kampeni hiyo, msaada wa
kisheria unatolewa bure katika Halmashauri zote saba za Mkoa wa Singida hadi
tarehe 19 Januari, 2024, lengo likiwa ni kufikia jumla ya Kata 70 na vijiji
210. Hivyo wananchi wote wa Mkoa wa Singida kwenye kata ambazo kampeni
hiyo itafanyika wameombwa kuitumia fursa hiyo kwa kuhakikisha kuwa wanashiriki
kikamilifu kwa kupata elimu na huduma
mbalimbali za masuala ya kisheria
zitakazotolewa. Aidha, amewasihi viongozi wa maeneo hayo kutoa
ushirikiano wa kutosha kwa wataalam wanaotekeleza kampeni.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkuu
wa Mkoa wa Singida Bw. Peter Serukamba amesema mkoa ulianza maandalizi ya
kuipokea kampeni tangu ilipozinduliwa mwezi Aprili 2023 Jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa kila Halmashauri ina watoa huduma ambao wamepata mafunzo ya
kutekeleza kampeni hiyo hivyo wataitumia fursa hiyo ipasavyo kwa mustakabali wa
kuendeleza amani ya mkoa na kumaliza migogoro inayochelewesha shughuli za
maendeleo.
Comments
Post a Comment