TUTAENDELEA KUTOA ELIMU NA KUTATUA CHANGAMOTO ZA KISHERIA KWA WANANCHI
Katibu Tawala wa Wilaya Singida Bi. Naima Bakari Chondo, akiongea baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa MSLAC katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, tarehe 19 Januari, 2024.
Bi. Basuta Milanzi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
MSLAC katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwa Katibu Tawala wa Wilaya
Singida Bi. Naima Bakari Chondo, tarehe 19 Januari, 2024
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na William Mabusi – WKS Singida
Katibu Tawala wa Wilaya Singida
Bi. Naima Bakari Chondo ameahidi kutekeleza changamoto za wananchi ambazo
hazikutatuliwa katika kipindi cha kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia
ili kuendelea kutatua migogoro kwenye jamii.
Bi. Naima ametoa kauli hiyo baada
ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Kampeni hiyo iliyokuwa inafanyika kwenye
Halmashauri yake kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Singida, tarehe 19 Januari,
2024.
Aidha, akiongelea changamoto za
kesi za ukatili wa kijinsia amesema, “ipo changamoto ya kesi za ukatili wa
kijinsia na kuzifanya kuwa ngumu kuendesha na wakati mwingine kutofika mwisho
kutokana na Mahakama kukosa ushahidi wakati ni kweli kabisa kitendo cha ukatili
kimefanyika, niwaombe waathirika na wazazi kutokukubali kumaliza kesi kifamilia,
maamuzi ya namna hii hayamtendei haki mwathirika.”
Katika hatua nyingine Mkurugenzi
Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Singida Bi. Esther Chaula amesema kwa kutumia
rasilmali kidogo waliyonayo wataendelea na utoaji elimu ya sheria kwa wananchi.
“Maeneo yaliyobaki tutajipanga na
watu wangu kwa kadri tutakavyoweza kutumia rasilmali tuliyonayo na kupitia
mikutano kutoa elimu ya kisheria na kuendelea kutatua migogoro kwenye jamii.
Unakuta mwananchi hakuridhika na uamuzi wa Mahakama, kwa kutokujua masuala ya
sheria anarudi tena Halmashauri. Wakati mwingine mwananchi anafanyiwa ukatili
bila kujua ni ukatili na wakati mwingine hata akijua ametendewa ukatili hajui
afanye nini.” Alisema Bi. Chaula.
Ameshukuru Wizara ya Katiba na
Sheria akisema kitendo cha kuwafuata
wananchi kuwapa elimu na huduma ya msaada wa kisheria kinawadhihirishia kwamba
Serikali iko karibu na wananchi. “Kupitia hii kampeni mmetuongezea maarifa
kwani watumishi mliokuwa mnazunguka nao kutekeleza kampeni kuna jambo
wamejifunza, hivyo tutawatumia kufika maeneo ambayo hamkuweza kufika.”
Kampeni ya Kitaifa ya kutoa elimu
na huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid Campaign
ilizinduliwa Mkoani Singida na Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana tarehe 10 Januari, 2024 na
kufanyika kwa siku kumi kwenye Halmashauri zote saba za mkoa huo na leo ndiyo
imehitimishwa.
Comments
Post a Comment