WANANCHI MKOANI SINGIDA WAENDELEA KUNUFAIKA NA MSLAC
Kaimu
Mkurugenzi wa Kitengo cha Msaada wa Kisheria Wizara ya Katiba na Sheria Bi.
Ester Msambazi akitoa huduma ya kisheria kwa Bw. Kimweri Stambuli alipotembelea
banda la Wizara kwenye viwanja vya Stendi ya zamani kupata huduma ya msaada wa
kisheria, tarehe 11/01/2024, Singida.
Wananchi
wanaotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria kwenye viwanja vya Stendi ya
zamani wakipatiwa huduma ya msaada wa kisheria, tarehe 11/01/2024, Singida.
Mratibu wa MSLAC Halmashauri ya Mkalama Bw. Antony Elias akitoa elimu ya sheria kwa wananchi wa Kata ya Mpambala, 12/01/2024, Singida.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na William Mabusi – WKS Singida
Kampeni
ya utoaji wa elimu ya sheria na huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia
Legal Aid Campaign (MSLAC) imeendelea kutoa nafuu kubwa kwa wananchi wa mkoa wa
Singida katika kukabiliana na changamoto mbalimbali hususan za kisheria.
Bw.
Kimweri Stambuli wa kijiji cha Iguguno ametembelea banda la Wizara ya Katiba na
Sheria lililopo Stend ya zamani kupata huduma ya msaada wa kisheria na kupatiwa
ufumbuzi wa shauri lake lililodumu kwa miaka tisa sasa.
“Msaada
huu ni utatuzi wa kero zinazomkabili mwananchi wa kawaida katika nchi hii,
shauri langu lilikuwa na mizengwe ya kusikilizwa kwa sababu sikuwa na Wakili,
lakini kupitia kampeni hii nimepata Wakili.” amesema Bw. Stambuli huku
akisisitiza kampeni hiyo ifanyike nchi nzima kutatua malalamiko ya wananchi ambayo
wengine wanashindwa wayapeleke wapi kutokana na kuwa mbali na vyombo vya
kutolea haki.”
Katika
hatua nyingine wakazi wa Kata ya Mpambala Halmashauri ya Mkalama wameshukuru
kampeni hiyo kwa kuwapa uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria hususan umiliki
wa ardhi kisheria kwani wamekuwa wakipokonywa mashamba yao na wananchi wachache
wajanja ambao wamekuwa wakitumia mwanya huo kujinufaisha kwa kuwapora maeneo
yao.
Mratibu
wa utekelezaji wa MSLAC kwenye Halmashauri ya Mkalama Bw. Antony Elias amesema
baada ya kukamilika kwa Kampeni hiyo timu yake itatoa majumuisho kwenye vyombo
husika kuhusu maeneo yote ambayo wananchi wamelalamikia ili hatua stahiki
zichukuliwe ili anayestahili haki apate haki yake bila kujali unyonge wake au
kutokujua sheria.
Mtendaji
Kata ya Mpambala Bw. Shadrack Makala, amekili kuwepo kwa matukio ya wananchi
kupokonywa mashamba yao na kuwataka watoe ushahidi watakapoombwa kufanya hivyo
ili wanaoshiriki vitendo vya uvunjifu wa sheria wachukuliwe hatua.
Naye
Bw. Martine Mbasha mkazi wa kijiji cha Ipande kata ya Ipande akiwa kwenye
mkutano wa utekelezaji wa MSLAC katika Halmashauri ya Itigi amesema Kampeni ya
huduma ya kisheria ya Mama Samia imekuwa msaada mkubwa sana “tumefurahia elimu
ya uandishi wa wosia na hasa utunzaji wake, hatukujua wosia unaweza kutunzwa na
vyombo vingine kisheria lakini sasa tumeelewa wosia unatunzwa RITA tofauti na
hapo wosia unaweza kuchanwa au kubadilishwa.”
Utekelezaji wa
Mama Samia Legal Aid Campaign (MSLAC) umezinduliwa mkoani humo na Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana tarehe 10 Januari, 2024 na
itatekelezwa kwa siku kumi katika Halmashauri zote saba.
Comments
Post a Comment