WANANCHI WASHAURIWA KUIBUA KERO NZITO NZITO KUITWISHA MSLAC
Afande Veronica Masele kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Halmashauri ya Wilaya ya Singida akitoa mada ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Ikhanoda, 16 Januari, 2024.
Afisa Ardhi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Singida Bi. Paskazia Kyaruzi akitoa mada kuhusu masuala ya ardhi,
tarehe 16 Januari, 2024 Kijiji cha Ikhanoda.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na William Mabusi –
WKS Singida
Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Kijiji cha Ikhanoda Kata ya Ikhanoda katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida
Bw. Jumanne Idabu amewataka wananchi kuibua kero ambazo zimeshindika na
kuitwisha Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Legal Aid Campaign (MSLAC)
ili zitatuliwe.
Bw. Idabu alitoa kauli hiyo
kwenye mkutano wa kutekeleza kampeni hiyo uliofanyika kijijini hapo tarehe 16
Januari, 2024 ukihudhuriwa na wakazi wa vijiji vya Ikhanoda na Msimihi.
“Wananchi ibueni kero nzito
ambazo walau zimeshachukuliwa hatua katika ngazi mbalimbali bila mafanikio ili
Kampeni hii itusaidie,” alisema.
Katika mkutano huo wananchi
walilalamikia Kampuni ya Majembe Auction Mart kushindwa kubomoa nyumba za
mwanakijiji mwenzao ambaye amemega na kujimilikisha eneo la shule ya Msingi ya
Ikhanoda lenye ukubwa wa hekari kumi na saba. Maamuzi kuhusu mgogoro huo
yalishaamuriwa na Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Singida tarehe 14 Machi,
2022. Halmashauri ya Kijiji iliamua kuingia mkataba na Majembe Auction Mart
baada ya mvamizi huyo kushindwa kuondoka kwa hiari baada ya siku kumi na nne
alizokuwa amepewa na Baraza.
Akithibitisha kero hiyo Bw. Idabu
amesema viambatisho vyote, kuanzia kushinda shauri hilo hadi vya malipo ya
gharama za ubomoaji kwa kampuni ya Majembe wanavyo. Kampuni hiyo imelipwa
gharama hizo tangu mwezi Desemba 2022.
Akijibu swali hilo kwa niaba ya
timu ya MSLAC inayotekeleza kampeni kwenye Halmashauri hiyo, Mwanasheria wa
Halmashauri ya Wilaya ya Singida Bi. Lela Salum amesema kero hiyo ameichukua na
itafikishwa vyombo husika ili Majembe Auction Mart wachukuliwe hatua.
Awali akitoa mada ya ardhi Afisa
Ardhi wa Halmashauri hiyo Bi. Paskazia Kyaruzi alishauri wamiliki wa ardhi
kuhakikisha wana hati za umiliki wa maeneo yao zinazotolewa na Serikali.
Akitaja faida za umiliki wa ardhi yenye hati kuwa ni pamoja na kupandisha
thamani ya ardhi, kuepusha migogoro na pia hati kutumika kama dhamana ya mkopo
benki.
Kampeni hiyo ya Kitaifa iliyozinduliwa kutekelezwa kwenye Halmashauri zote mkoani humo na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana tarehe 10 Januari, 2024 itafikia tamati tarehe 19 Januari, 2024.
Comments
Post a Comment