CHETI CHA KUZALIWA SIO KIGEZO PEKEE CHA URAIA
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
akizungumza na Watendaji wa Ofisi ya RITA ya Njombe, 27 Januari, 2024
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Ofisi ya RITA Njombe Mjini, 27
Januari, 2024.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Na Lusajo Mwakabuku -
Njombe
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
amesema cheti cha kuzaliwa hakimpi mtu yeyote uhalali wa uraia wake bali ni
uthibitisho wa kuzaliwa kwake au kinaweza kutumika kama moja ya kigezo cha
kuthibitisha uraia.
Waziri Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo wakati alipotembelea
Ofisi za Msajili wa Vizazi na Vifo Mkoa wa Njombe kwa lengo la kuangalia hali
uandikishaji usajili wa watoto chini ya miaka mitano, tarehe 27 Januari, 2024.
“Sio uthibitisho pekee na ndiyo maana cheti cha kuzaliwa
hata mtoto ambaye wazazi wake wote wawili sio watanzania ni wageni wamekuja
kutalii akizaliwa Tanzania atapata cheti hivyo katika vigezo vyetu vya
kuangalia huyu ni Mtanzania ama sio Mtanzania cheti cha kuzaliwa kinaweza
kikatumika lakini sio guarantee pekee,” alisema Dkt. Chana.
Alisema kuwa cheti cha kuzaliwa kinathibitisha kwamba mtu
huyu ni mzaliwa nchini Tanzania lakini sio hakikisho la mwisho kwamba wewe ni
mzawa.
“Tukija kwenye utaratibu wa uraia kuna taratibu zake, kuna
sheria zake za kutambua kwamba huyu je ni Mtanzania au sio Mtanzania hivyo
niwakumbushe cheti cha kuzaliwa kinaonyesha mtoto amezaliwa wapi na habari za
uraia kuna taratibu nyingine,” alisema Dkt. Chana.
Balozi Dkt. Chana alisema kila mtoto Mtanzania anapozaliwa
anayo haki ya kupata cheti cha kuzaliwa kwa sababu ni haki ya kila mmoja.
“Watanzania wenzangu, wamama wenzangu tunapokwenda katika
zahanati, hospitali na hivi sasa tupige marufuku kabisa watu kujifungulia
nyumbani, watu wanatakiwa kujifungulia katika vituo vya afya tumejenga tunavyo
vya kutosha na hivyo mtoto anapozaliwa hakikisha kabla ya kuondoka kwenda
nyumbani unapata cheti chako cha kuzaliwa cha mtoto,” alisema Waziri Chana.
Alisema Serikali imedhamiria kwamba tangu mwaka 2020 hadi
2025 kila mtoto anayezaliwa na watoto wote wanatakiwa kuwa na vyeti vya
kuzaliwa.
“Tatizo ni nini Watanzania wenzangu, shida ni nini ni haki
yako chini ya umri wa miaka mitano tena unapata bure Mhe. Rais Samia Suluhu
Hassan ameshafadhiri lakini wale wa umri ambao umezidi miaka mitano pia cheti
cha kuzaliwa ni haki yako lakini kuna malipo kiasi fulani kidogo ambacho
unapaswa kulipa ili upate cheti chako,” alisema.
Pia waziri amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha
kwamba wanatenga fedha kwa ajili ya kuwezesha shughuli za usajili wa watoto chini
ya miaka mitano.
Awali Mratibu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini RITA
Mkoa wa Njombe, Rahabu Daud alisema mpango wa usajili wa watoto chini ya miaka
mitano katika mkoa wa Njombe ulianza kutekelezwa kuanzia Septemba 2016 hadi
hivi sasa jumla ya watoto 190,075 wamesajiliwa na kupatiwa vyeti hadi kufikia
Januari 25 mwaka 2024.
“Watoto hawa waliosajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa
wakati wakiwa na umri wa chini ya miaka mitano na kiwango cha usajili katika
mkoa kimeongezeka kutoka asilimia 8.6 (Sensa 2012) hadi kufikia asilimia 64.9
Januari 2024,” alisema Daud.
Alisema kabla ya kutekeleza mpango huo Halmshauri za wilaya
za Njombe, Ludewa na Wanging’ombe hali ya usajili ilikuwa asilimia sita mwaka
2012 na kufikia Januari 2024 hali ya usajili umeongezeka kwa wastani wa
asilimia 65.
Comments
Post a Comment