BUNGE LARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MAPENDEKEZO INAYOTOA KWA SERIKALI
Mkurugenzi wa Utawala na
Rasilimaliwatu Bw. Michael Masanja akimkaribisha Naibu
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda kuongea na
Wataalamu wa Wizara kujadili majibu ya mapendekezo ya Bunge, tarehe 13
Februari, 2024 Bungeni Dodoma.
Baadhi ya Wakurugenzi wa
Wizara ya Katiba na Sheria walioshiriki katika kikao cha kuandaa majibu ya mapendekezo ya Bunge, tarehe 13
Februari, 2024 Bungeni Dodoma.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na William Mabusi – WKS Dodoma
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama amesema Bunge
linaridhishwa jinsi Serikali inavyotekeleza ushauri na mapendekezo yanayotolewa
na Bunge kupitia Kamati mbalimbali za Kudumu.
Dkt. Mhagama amesema hayo leo
tarehe 13 Februari, 2024 alipokuwa anasoma Taarifa ya Mwaka ya Shughuli
za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria katika kipindi cha
kuazia Februari, 2023 hadi Januari, 2024. Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge
husimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wizara tano ikiwemo Wizara ya
Katiba na Sheria.
“Kwa sehemu kubwa, Kamati
imeridhishwa na utekelezaji wa maazimio ya Bunge uliofanywa na Wizara na
taasisi zake. Kwa yale maeneo ambayo yanahitaji kutiliwa mkazo zaidi katika
utekelezaji wake, Kamati imetoa ushauri mahsusi ili yakafanyiwe kazi zaidi.” Alisema.
Ameyataja mapendekezo hayo
kuwa ni pamoja na Serikali kuendelea kuboresha majengo ya Mahakama za Mwanzo
yanayostahili kuboreshwa ama kujenga mapya na kuwekwa miundombinu ya TEHAMA
itakayowezesha Mahakama hizo kutoa huduma za TEHAMA kama ilivyo kwenye Mahakama
zingine, Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya Taasisi za mfumo wa Haki
Jinai na kuajiri watumishi wa kutosha kwenye Taasisi hizo kwa kuzingatia Ikama.
Akijibu mapendekezo hayo kwa
niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amesema Serikali
kwa kushirikiana na Mahakama inaendelea na Mpango wa ujenzi wa majengo ya
Mahakama za Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini ili kusogeza huduma karibu
na wananchi. Chini ya Mpango huo katika mwaka wa fedha 2023/24 zinajengwa
Mahakama za Mwanzo 72 katika mikoa mbalimbali. Aidha, kwa kuzingatia
Mpango wa Ujenzi wa Mahakama, mwaka wa fedha 204/25 Mahakama za Mwanzo 32
zinatarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akijibu pendekezo la kuwekwa miundombinu ya TEHAMA kwenye Mahakama za Mwanzo, Mhe.
Pinda amesema majengo mengi ya Mahakama za Mwanzo yapo maeneo ambayo hayajafikiwa na
mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, na hivyo kushindwa kuunganishwa kwenye
miundombinu ya moja kwa moja. Kwa sasa katika kukabiliana na changamoto hiyo,
Mahakama imetengeneza mfumo maalum wa Mahakama za Mwanzo (Primary Court Mobile
App) ambao unawezesha kutunza takwimu na kumbukumbu za mashauri yanayoendeshwa
katika Mahakama hizo.
Kuhusu mapendekezo ya Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya Taasisi za mfumo wa Haki Jinai amesema Serikali itaendelea kuomba ongezeko la bajeti na ongezeko la watumishi katika taasisi hizo kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Katika kipindi hicho jumla ya miswada 12 ilichambuliwa na Kamati kutoa mapendekezo ya Bunge, Kamati ilitembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotengewa fedha katika Mwaka wa Fedha 2022/2023. Aidha, Kamati ilifanya uchambuzi wa utekelezaji wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na kujiridhisha na matumizi ya bajeti hizo.
Comments
Post a Comment