TEKELEZENI KWA UKAMILIFU MFUMO WA UTOAJI MSAADA WA KISHERIA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia Siku ya Sheria, tarehe 01 Februari, 2024 Jijini Dodoma.
Bi. Mary Makondo Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria akisalimiana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria, 01 Februari, 2024, Jijini Dodoma.
Na William Mabusi – WKS Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kwa
kushirikiana na Wadau wengine kutekeleza kwa ukamilifu mfumo wa utoaji huduma
ya msaada wa kisheria kwa wanachi hasa wanyonge kupitia Kampeni ya Kitaifa ya
Mama Samia Legal Aid Campaign ili kuwatatulia migogoro mbalimbali
wanayokabiliana nayo.
Dkt. Samia ameyasema hayo
alipokuwa akihutubia kwenye kilele cha Siku ya Sheria nchini leo tarehe 01
Februari, 2024 kwenye viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma.
“Tunashukuru sana kwani kwenye
mikoa sita ambako kampeni imetekelezwa imepokelewa vizuri kwa wananchi, na kwa
jinsi ilivyopokelewa ni wazi kuwa kuna uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria
hapa nchini. Naiagiza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Wadau wengine
kutekeleza kwa ukamilifu mfumo wa utoaji msaada wa kisheria kwa mujibu wa
sheria.” Amesema na kuongeza “Mazingira ya jamii yetu yalitulazimu kuanzisha
programu hiyo ili wananchi wasio na uwezo kupitia kampeni hiyo wapatiwe msaada
wa kisheria.”
Utekelezaji wa kampeni hiyo
umesaidia kubaini maeneo yenye malalamiko makubwa ambayo ni pamoja na migogoro
ya ardhi, mirathi, ukatili wa kijinsia, ndoa na matunzo kwa watoto.
Katika hatua nyingine Mhe.
Rais amesisitiza juu ya matumizi ya kuamua kesi kwa njia mbadala, “tuweke
kipaumbele katika kuamua kesi kwa njia ya usuluhishi, kwani pande zinazohusika
zikifikia maridhiano huepuka mapingamizi mengi katika uendeshaji wa kesi
mahakamani. Shauri linaloisha kwa njia ya usuluhishi haliachi makovu kwa
wahusika kuchukiana na hivyo wahusika kubaki wakiendelea kushirikiana katika
kazi.”
Mhe. Rais akatoa wito kwa Vituo
vya Sheria na Shule ya Sheria kuongeza kasi ya kuandaa wataalam katika tasnia
ya usuluhishi nchini, vile vile akaitaka Wizara Katiba na Sheria kukaa na Wadau
wa usuluhishi kubainisha maeneo yanayotakiwa kufanyiwa kazi ikiwemo hitajio la
kutunga Sera ya usuluhishi.
Awali akimkaribisha Mgeni
Rasmi, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma, amesema utashi wa kisiasa unaooneshwa na Mhe. Rais
Dkt. Samia umechangia kuboresha haki na haki jinai nchini, akitaja mifano
michache amesema kuundwa kwa Tume ya Haki Jinai, kuanza kwa Kampeni ya Mama
Samia ya Msaada wa Kisheria ni miongoni mwa ishara za utashi wa Kiasa wa Mhe.
Rais.
Comments
Post a Comment