WIZARA KUENDELEA KUBORESHA SHERIA – DKT. CHANA
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Balozi Dkt. Pindi Chana akijibu maswali, tarehe 02 Februari, 2024 Bungeni
Dodoma.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na William Mabusi – WKS Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi
Chana amesema Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kuzifanyia
utafiti na kuboersha sheria zote zinazotakiwa kufanyiwa mabadiliko.
Dkt. Chana amesema hayo alipokuwa akijibu swali la
Mbunge wa Tabora Mjini Mhe. Emmanuel Adamson Mwakasaka, aliyetaka
kujua lini Serikali italeta Bungeni Sheria mahsusi kwa ajili ya kuwalinda
wananchi dhidi ya Ukatili wa Kijinsia.
Amesema “tunazo Sheria zinazowalinda wananchi dhidi
ya ukatili wa kijinsia ambazo ni Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, Sheria
ya Ndoa Sura ya 29, Sheria ya Mtoto Sura ya 13, Sheria ya Makosa ya Mtandao
Sura ya 443 na Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu Sura ya 432.
Kwa pamoja Sheria hizo zina vifungu vinavyozuia makosa ya ukatili wa kijinsia,
zote kwa pamoja zina vifungu vinavyoshugulika na makosa ya ukatili wa kijinsia.
Hata hivyo, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara nyingine za kisekta ikiwemo
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Makundi Maalum, Wizara ya Mambo
ya Ndani ya Nchi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na wadau mbalimbali tunaendelea
na uchambuzi ili kubaini iwapo ipo haja ya kuwa na sheria mahsusi ya ukatili wa
kijinsia au tuboreshe sheria zilizopo. Baada ya kukamilika kwa uchambuzi huo Serikali
itachukua hatua stahiki.”
Aidha, Dkt. Chana amewataka
Wananchi kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia Vituo vya Polisi bila hofu ili
sheria ichukue mkondo wake huku akisisitiza kuwa watoa taarifa na mashahidi nao
wanalindwa na sheria ya kuwalinda Watoa taarifa na Mashahidi ya mwaka 2015.
Akijibu swali la Mbunge wa
Ukerewe Mhe. Joseph Michael
Mkundi aliyetaka kujua lini Serikali itakarabati na kujenga Mahakama mpya ya
Wilaya ya Ukerewe. Dkt. Chana amesema Serikali
kupitia Mahakama ina mpango wa kujenga na kuboresha majengo ya Mahakama katika
ngazi mbalimbali, katika utekelezaji wa mpango huo Serikali imepanga
kujenga Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe katika mwaka wa fedha 2024/25.
Comments
Post a Comment