DKT. CHANA AHIMIZA USHIRIKIANO NA UWAJIBIKAJI
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Baraza Bi.
Mary Makondo akihutubia kwenye Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo,
tarehe 21 Machi, 2024 Jijini Dodoma.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa Halmashauri ya TUGHE tawi la Wizara baada kuhutubia Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, tarehe 21 Machi, 2024 Jijini Dodoma.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na William Mabusi – WKS
Dodoma
Waziri
wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewataka watumishi wa Wizara
ya Katiba na Sheria kuongeza ushirikiano na kila mmoja kutimiza wajibu wake ili
kwenda na kasi ya maboresho na mapinduzi makubwa yaliyofanyika ndani ya kipindi
cha miaka mitatu ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo
kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ya kuboresha mfumo wa utoaji haki.
Dkt.
Chana ameyasema hayo wakati anafungua Kikao cha Kwanza cha Baraza la Nane la
Wizara hiyo tarehe 21 Machi, 2024 Jijini Dodoma ambako alialikwa kama Mgeni
Rasmi.
“TUGHE
ni kiunganishi cha Watumishi na Menejimenti, tuongeze ushirikiano katika
kutekeleza majukumu yetu. Kila mtumishi anapashwa kujua wajibu wake na kuutimiza
kwa mujibu wa Kanuni na Miongozo ya Utumishi wa Umma bila kusahau kuwa Wizara
yetu ni catalyst kwa Wizara zingine. Sisi ni wale ambao tunachochea Wizara na Taasisi
nyingine kufanya kazi vizuri, utungaji wa sheria na maboresho yake ni suala
ambalo linatutegemea endapo kutakuwa na haja ya kufanya hivyo.” Alisema.
Amesisitiza
kufanyika kwa vikao vya Baraza kwa mujibu wa Mkataba wa kusimamia Baraza la Wafanyakazi
huku akiagiza kufanyika kwa vikao vya Idara na Vitengo pia.
“Serikali
inazingatia umuhimu wa kuwepo kwa Mabaraza ya Wafanyakazi na kufanyika kwake
kwa mujibu wa Mikataba inayounda Mabaraza hayo. Mabaraza ni jambo la kisheria
lakini pia yana kazi ya kushauri namna ya kuboresha utendaji kazi, hivyo ni
vema vikao hivyo vikafanyika kadri sheria inavyotaka.” Alisema Dkt. Chana na
kuongeza;
“Mada
zinazojadiliwa kwenye vikao vya Baraza ni namna ya kuwashirikisha watumishi
kuhusu nini kinafanyika mahala pao za kazi. Aidha, kwenye vikao vya Mabaraza
ndiko zinakoelezwa changamoto za watumishi na namna ya kuzitatua, fursa hizi
hutumika pia kupunguza msongo wa mawazo, hivyo tutumie fursa hii vizuri.”
Akimkaribisha
Mgeni Rasmi kuhutubia Baraza hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ambaye pia ndiye
Mwenyekiti wa Baraza Bi. Mary Makondo aliwataka wajumbe wa Baraza kujali
maslahi ya Taifa katika kutekeleza majukumu yao, “tutekeleze majukumu yetu kwa
ustawi wa Taifa, wananchi wahudumiewe kwa huduma ambazo zimeboreshwa. Haki si
tu iwepo bali ionekane inatendeka,” alisema.
Akisoma
taarifa ya TUGHE, Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Wizara Bw. William Mabusi aliomba
kuwepo na hafla ya kuwaaga watumishi wanaostaafu kwa mujibu wa sheria, “Utumishi
wa Umma ni safari ndefu yenye milima na mabonde ambayo wote tunayafahamu,
tunaomba uwepo utaratibu wa kuwaaga watumishi hao ikiwa ni namna ya kuwapa
pongezi, kutambua mchango wao katika utumishi wa umma na kuongeza mshikamano na
upendo katika ofisi.”
Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza Bi. Makondo aliwaasa Watumishi kutekeleza majukumu yao si kwa kujifikiria wao wenyewe, “tusijifikirie sisi tu, kuna Watanzania huko mtaani, kuna yatima huko, wapo wasio kuwa na uwezo tuwatembelee mara moja moja na kuwasaidia.” Alisema huku akiagiza utekelezaji wa mazimio ya Baraza, “maazimio ya Baraza hili yafanyiwe kazi, mara zote tunakumbushwa hakuna haki bila wajibu.”
Comments
Post a Comment