KAMATI YA BUNGE YAKAGUA MRADI WA UJENZI WA IJC NJOMBE
Waziri wa Katiba na
Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza na Wanahabari wakati wa
ukaguzi uliofanywa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria
kwenye Mradi wa ujenzi wa IJC mkoani Njombe. Tareh 13 Machi, 2024.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Kizito Mhagama (wa pili
kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ukaguzi wa Mradi wa Ujenzi
wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) mkoani Njombe tarehe 13 Machi, 2024.
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakichangia wasilisho la taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kinachojengwa mkoani Njombe na Mahakama ya Tanzania. Tarehe 13 Machi, 2024.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Lusajo Mwakabuku – WKS, Njombe.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala,
Katiba na Sheria tarehe 13 Machi, 2024 imekagua Mradi wa Ujenzi wa Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki IJC kinachojengwa mkoani Njombe chenye thamani ya
shilingi takribani Bilioni 7.6 mradi unaotekelezwa na Mahakama ya Tanzania.
Akizungumza wakati wa zoezi la
ukaguzi wa kituo hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba
na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Kizito Mhagama amesema mradi huo ni moja ya miradi
mikubwa inayotekelezwa nchini kupitia Wizara ya Katiba na Sheria na Mtekelezaji
wa mradi ni Mhimili wa Mahakama.
“Mradi huu ni wa kutoa huduma
za sheria kwenye jengo moja ‘Integrated Justice Centre’ ambapo Mahakama za
ngazi mbalimbali zinakuwa katika jengo moja ili kurahisisha upatikanaji wa haki
kwa wananchi lakini pia wanaotoa haki waweze kutekeleza wajibu wao na majukumu
yao kwa namna ambayo ni jumuishi na rahisi zaidi,” ameeleza Mhe. Dkt. Mhagama
na kuongeza kuwa;
“Hii ni hatua kubwa sana ya
kuboresha mifumo ya utoaji haki nchini ikizingatiwa kwamba, tunaendelea
kuijenga Tanzania ambayo ina hali ya utulivu na amani ya kutosha,” amesema Mhe.
Mhagama.
Aidha, Mhe. Dkt. Mhagama amesema
kuwa, kwakuwa mradi huo umeshuhudiwa na Wabunge wa Kamati hiyo kwa pamoja ni
imani yao kuwa changamoto zozote zitakazojitokeza zitatolewa taarifa kwa
ukaribu zaidi ili wakati wa kupanga bajeti zisaidie kutatuliwa kwa mwaka ujao
wa fedha ambao utahusu pia uendelezaji na ujenzi wa miundombinu ya utoaji haki
kwa Watanzania.
Kamati imempongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuthubutu na
kwa kuamua kwa dhati kabisa kusogeza huduma ya utoaji haki kwa wananchi wa
Tanzania ambao wanahitaji huduma hiyo inayotekelezwa mkoani Njombe na maeneo
mengine nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema ukaguzi huo wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria unaenda sambamba na maelekezo ya Rais
Samia ya kuboresha miundombinu ya utoaji haki kwa maana ya “Reforms &
Rebuilding” ili Watanzania wote wapate haki kwa usawa na kwa wakati kama
ilivyokusudiwa.
“Kamati hii ya Bunge
inatusaidia sana mawazo na mapendekezo ya namna bora ya kuboresha shughuli za
utoaji haki kupitia Serikali na Mahakama. Tunajua jukumu la Bunge ni kupitisha
bajeti, kutunga sheria na kuisimamia Serikali, hivyo leo tupo katika jukumu
mojawapo la Bunge la kusimamia Serikali ‘Oversight role’ ya kupitia Kamati ya
Bunge baada ya kupitisha Bajeti hii ndiyo kazi ya Kamati,” amesema Mhe. Dkt.
Chana.
Mhe. Dkt. Chana amesema,
Wizara ya Katiba na Sheria imedhamiria kuhakikisha utawala wa sheria unakuwa ni
miongoni mwa vipaumbele vya Serikali.
“Tunataka kuona wawekezaji wanakuwa
na imani na Utawala wa Sheria, tunataka Watanzania waishi kwa amani, kwa uhuru
bila kuwepo na changamoto za kijinai na pale zinapojitokeza basi tuwe na
miundombinu ya kudhibiti na kukabiliana nazo,”
Mhe. Dkt. Chana ameongeza kuwa
miundombinu hiyo inayojengwa inakwenda sambamba na matumizi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia
Duniani hasa katika eneo la utoaji haki, ikiwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa
IJC Njombe.
Naye,
Mkadiriaji Majengo kutoka Mahakama ya Tanzania, Bw. Abdallah Nalicho akifanya
wasilisho fupi la Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC)
mkoani Njombe, amesema kuwa ujenzi wa kituo hicho umezingatia mahitaji
mbalimbali yanayoendana na uhalisia na matarajio ya wananchi watakaopata huduma
za haki ndani ya jengo hilo. Matarajio hayo ni pamoja na kupunguza gharama za
uendeshaji wa mashauri, kuokoa muda na kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa watoa
haki.
“Mathalani
usanifu wa jengo hili umezingatia mahitaji ya watu wenye mahitaji maalum mfano;
walemavu, watoto, akina mama wanaonyonyesha na wajawazito, wazee wasiojiweza na
wadau mbambali katika mnyororo wa utoaji haki wanaosaidiana na Mahakama (Waendesha
Mashtaka, Mawakili wa kujitengemea, Watoa ushauri wa kisheria, Ustawi wa Jamii,
Dawati la jinsia na Mahakama maalum kwa ajili ya watoto waliokinzana na
Sheria,” ameongeza Bw. Nalicho.
Akielezea
faida za ziada za ujenzi wa Kituo hicho, Bw. Nalicho amesema kimesaidia kutoa
ajira kwa wataalum wa masuala ya ujenzi wapatao 23 na wafanyakazi wasio
wataaluma wa ujenzi wenyeji wa Mkoa wa Njombe na hivyo kukuza na kuongeza
kipato cha wananchi kupitia Mradi huo.
Comments
Post a Comment