KAMATI YAIDHINISHA BAJETI YA MAHAKAMA KWA MWAKA WA FEDHA 2024/25
Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel akisoma Makadirio ya bajeti ya Mahakama kwa mwaka wa fedha 2024/25 mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, tarehe 18 Machi, 2024 Ofisi za Bunge Dodoma.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. Dkt. Charles Kimei akichangia hoja baada ya Kamati hiyo kupokea Makadirio ya bajeti ya Mahakama kwa mwaka wa fedha 2024/25, tarehe 18 Machi, 2024 Ofisi za Bunge Dodoma.
Waziri
wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (kulia) akisoma taarifa wakati wa Kikao cha Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, tarehe 18 Machi, 2024 Ofisi za Bunge Dodoma.
Na William Mabusi – WKS Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Bajeti ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Daniel Sillo imepokea na kuidhinisha
Makadirio ya bajeti ya Mhimili wa Mahakama kwa mwaka wa fedha 2024/25 ikiwa ni ongezeko
la asilimia 10.67 kutoka bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 huku wakiutaka
mhimili huo kuongeza Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) na kupanua wigo wa
matumizi ya mfumo wa Unukuzi na Tafsiri wa Mwenendo wa Mashauri ya Mahakama (Transcription
and Translation System - TTS).
Akisoma Makadirio ya bajeti
hiyo mbele ya Kamati tarehe 18 Machi, 2024 Ofisi za Bunge Dodoma, Mtendaji Mkuu
wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel ameyataja baadhi ya maeneo ya kipaumbele
kuwa ni pamoja na Kuongeza Mobile Courts sita, Kuendelea kupunguza mrundikano
wa mashauri mahakamani (backlogs), Kukamilika ujenzi wa Vituo sita Jumuishi vya
Utoaji Haki (ICJ). Aidha, bajeti hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa utendaji
kazi na kuimarisha mafunzo kwa watumishi.
Akichangia kwenye kikao hicho
Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. Charles Kimei amesema Mahakama iweke mkakati wa
kuendelea kusimika mfumo wa TTS kwenye Mahakama zingine nchini kwani hadi sasa
ni Mahakama 11 tu zinazotumia mfumo huo.
Katika uhitaji wa Mahakama
zinazotembea (Mobile courts) Dkt. Kimei amesema "Mobile court ziongezeke
basi mbona bado ni zile zile mbili, aidha Kamati ingependa kupata mrejesho wa
kuwepo kwa Mobile Wagon Court baada ya treni ya mwendokasi (SGR) kuanza kufanya
kazi.”
Akijibu hoja hiyo Mtendaji
Mkuu wa Mahakama amesema Mahakama imefikia makubaliano na Wizara ya Uchukuzi na
kwamba Mobile Wagon Courts zitaanza kutumika pale treni ya mwendo kasi itakapoanza
kufanya kazi. Na kuhusu kusimikwa kwa mfumo wa TTS amesema mfumo unaposimikwa
kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mahakama zote zilizoko katika Kituo hicho
kuanzia Mahakama ya Mwanzo hadi ya Rufani huunganishwa na mfumo.
Akitoa shukrani zake kwa
Kamati, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameihakikishia
Kamati kwamba kazi zote ambazo zimeombewa fedha zitatekelezwa kwa ufanisi
mkubwa “Mahakama za Mwanzo 72 zilizoombewa fedha zitajengwa kwa mwaka wa fedha
2024/25 lengo likiwa kuwa na Mahakama za Mwanzo karibu kila Kata ingawa
haziwezi kuwa Kata zote kwani Kata zingine hasa za mjini ziko karibu karibu ila
kwa Wilaya ni ndoto za Wizara kuona kila Wilaya inakuwa na Mahakama.
Katika taarifa yake kwenye
kikao hicho, Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali
itaendelea kutoa fedha kwa Mahakama ili kuhakikisha shughuli za mhimili huo
muhimu za utoaji haki zinatekelezwa kama ilivyopangwa, ikiwemo kugharamia Mahakama
mpya zilizokamilika kujengwa.
“Mahakama ndiyo taasisi inayokimbiliwa na wengi katika kutoa haki hivyo Serikali huwa inaihudumia kadri inayotakiwa na hata ikitokea dharula ambayo itapelekea kasi ya kupeleka fedha kwenye Mahakama kupungua ni lazima hata wao (Mahakama) watakubaliana na Serikali kwamba sababu hiyo ni ya msingi na ilipashwa itekelezwe kwanza.” Alisema Mhe. Mwigulu.
Comments
Post a Comment