KAMATI YAPOKEA NA KURIDHIA MAKADIRIO YA BAJETI 2024/25
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo akitoa salaam kwenye Kikao cha Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, baada ya Wizara yake kuwasilisha
Makadirio ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 tarehe 25 Machi, 2024 kwenye
Ofisi za Bunge Dodoma.
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakifuatilia wakati Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akiwasilisha Makadirio ya Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwenye Kamati hiyo, tarehe 25 Machi, 2024 Ofisi za Bunge Dodoma.
Na William Mabusi – WKS
Dodoma
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepokea na kuridhia Mpango wa
Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2024/25
huku ikiahidi kuitetea kwenye Bunge lijalo la Bajeti.
Makadirio ya bajeti hiyo
yamewasilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
tarehe 25 Machi, 2024 kwenye Ofisi za Bunge Dodoma. Katika kikao hicho Dkt.
Chana aliambatana na Katibu Mkuu Bi. Mary Makondo, Naibu Katibu Mkuu Dkt.
Khatibu Kazungu pamoja na Wakuu wote wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.
Akichangia baada ya
kuwasilishwa kwa makadirio hayo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Florent
Kyombo amesema, ”kwetu sisi kupokea makadirio haya ya bajeti siyo kwamba
tumemaliza kazi bali kazi ndiyo kwanza tumeianza kuhakikisha kwamba yale
tuliyokubaliana tunayasimamia na kuyatetea kadri itakavyowezekana ili
yapitishwe kwenye vikao vingine na yatekelezwe.”
Naye Mhe. Edward Olelekaita
Kisau ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati hiyo ameipongeza Wizara kwa utekelezaji wa
majukumu yake kadri ya ushauri wa Kamati huku akitoa wito kwa Serikali kuwapa
ushirikiano wa kutosha na kuendelea kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali kuwaongezea
ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.
”Tunaona Mawakili wa Serikali
wanashinda kesi nyingi na zenye pesa nyingi za ndani na hata za Kimataifa na
kuokoa kiasi kikubwa cha pesa, tunataka kuona Mawakili hao wakipewa ushirikiano
mkubwa, tuone Mawakili hawa walau wanapewe barua za ”recognition” tusiseme tu
uzalendo, uzalendo peke yake haitoshi. Mawakili binafsi wakipelekewa kazi kabla
ya kuchaji wanaangalia kiasi cha pesa watakachookoa halafu ndiyo wanachaji
gharama za kesi.”
Aidha, Kamati hiyo imeshauri
Serikali kuendeleza miradi ambayo imeshaanza kutekelezwa na tayari wananchi
wanafurahia utekelezaji wake hata kama Washirika wa Maendeleo wataonesha
kutoendelea kufadhili miradi hiyo kwenye bajeti ijayo. Walitaja Mradi kama usajili
wa watoto chini ya umri wa miaka mitano na Mama Samia Legal Aid Campaign
miongoni mwa miradi mingine.
Akitoa salaam katika kikao
hicho Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amesema Wizara
na Taasisi zake itaendelea kutekeleza majukumu sawa na matarajio ya wananchi.
“Tutaendelea kufuata maelekezo
ya Kamati katika kutekeleza majukumu ya sekta ya sheria ili wananchi wapate
matarajio makubwa ambayo wanayo kutoka Wizarani na Taasisi zinazosimamia haki.
Tunaendelea kupokea maelekezo yenu na ahadi yetu ni kwamba tutaenda
kuyatekeleza ili kufikia malengo ya bajeti. Aidha, katika kuziba pengo la
bajeti inayokadiriwa, Wizara itaendelea kubuni miradi ya maendeleo kwa
kushirikiana na Wadau wa Ndani na Nje na tayari mawasiliano kati yetu na Wadau
yameanza. Amesema Bi. Makondo.
Comments
Post a Comment