KAMATI YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kwenye picha ya pamoja na Waziri Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel, tarehe 13 Machi, 2024, walipotembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma.
Na William Mabusi – WKS
Dodoma
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph
Mhagama amesema Kamati imeridhishwa na matumizi ya fedha iliyoidhinishwa Bungeni
kutekeleza miradi mbalimbali ndani ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi
zake na kwamba Kamati iko tayari kupokea na kujadili makadirio ya Bajeti ya
Wizara hiyo mwaka wa fedha 2024/25.
Dkt.
Mhagama ameyasema hayo wakati Kamati ilipotembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji
Haki kilichopo jengo la Makao Makuu ya Mahakama Jijini Dodoma, tarehe 17 Machi,
2024, siku ya mwisho kwenye ziara ya Kamati kutembelea miradi ambayo pesa yake
ilipitishwa na Bunge kwenye bajeti ya mwaka 2023/24.
Katika
ziara hiyo Kamati imeoneshwa jinsi mfumo wa Kunukuu na Kutafsiri (Transcription
and Translation System - TTS) unavyofanya kazi ya kunukuu na kutafsiri mwenendo
wa uendeshaji wa mashauri ya Mahakama na taarifa yake kuchapishwa kwa muda
mfupi sana yaani ndani ya saa 12.
”Kazi
iliyokuwa inafanywa na Majaji ya kumsikiliza mtu halafu anaandika kwenye
karatasi ilikuwa inachukua muda mrefu sana kuandaa taarifa za mienendo ya mashauri
ya Mahakama. Lakini kwa kutumia mfumo huu hukumu inatoka ndani ya saa 12 haya ni mapinduzi
makubwa kwenye eneo la utoaji haki katika nchi yetu.” amesema Dkt. Mhagama na
kuongeza kuwa ”Bunge liko tayari kujadili bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha
2024/25 tukiamini bajeti ya mwaka 2024/25 itahusisha kuimarisha mifumo kama hii
kwenye Mahakama zetu.”
Pia
Dkt. Mhagama amesema, ”endapo mfumo huu utafungwa kwenye Mahakama zote nchini kuanzaia
Mahakama za Mwanzo hadi za Rufani tutakuwa tumesogeza huduma ya upatikanaji wa haki
kwa uhakika, kwa ufanisi na kwa wakati kwa watanzania walio wengi. Aidha, kutapunguza
muda wa kusubiri hukumu na yule anayetaka kukata rufaa baada ya hukumu, hivyo natoa
wito kwa Mahakama kuhakikisha mfumo unafungwa kwenye Mahakama zote nchini na
niiombe Serikali itangaze mfumo huu kwa nchi zote zinazotumia lugha ya Kiswahili
ili ziutumie na hapo nchi itakuwa imejiingizia mapato.”
Katika
ziara hiyo Kamati ilifanya majaribio ya mfumo huo katika kuendesha shughuli za
Bunge, jaribio ambalo lilionesha kuwa mfumo unaweza kutumika Bungeni kunukuu
vikao vya Bunge vya siku ambapo mazungumzo yote yatarekodiwa kisha kutafisiriwa
katika kuandaa taarifa mbalimbali kwa muda mfupi ikiwemo uandaaji wa hansadi.
Dkt. Mhagama akasema Bunge litaendelea kusoma mfumo huo ili lione jinsi gani unaweza
kuboreshwa ukaweza kutumika Bungeni kusaidia Bunge kufanya kazi za uwakilishi
wa wananchi, utungaji sheria na usimamizi wa Serikali kwa ufanisi.
Akiongea
katika ziara hiyo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana
ameishukuru Kamati kwa pongezi walizotoa kwa Wizara kwa kuridhishwa na
utekelezaji wa miradi ambayo Kamati imetembelea.
“Katika
ziara hii Kamati imepata fursa ya kutembelea Mahakama ya Mwanzo Mahenge, Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki Njombe, Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Ruvuma, na leo
mmejionea wenyewe kukamilika kwa kituo hiki Jumuishi cha Utoaji Haki na mfumo
wa TTS, nikuhakikishie Mhe. Mwenyekiti ushauri na mapendekezo ambayo Kamati
yako imetoa tutaendelea kuyafanyia kazi. Kwetu sisi hii ni bahati kupata fursa
ya kuonesha maboresho makubwa yanayofanywa na Wizara ikiwa ni jitihada za Mhe.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.”
Comments
Post a Comment